Jimi Wanjigi ajiunga na chama cha Safina baada ya kugura ODM

Muhtasari
  • Wanjigi alijiunga na chama cha Safina mnamo Jumatano
  • Alipokelewa kwa Safina na kiongozi wa chama na aliyekuwa mgombea urais Paul Muite
Jimi Wanjigi akizungumza baada ya kujiunga na chama cha Safina 9/Machi/2022
Image: Ezekiel Aming'a

Mfanyabiashara Jimi Wanjigi amegura chama cha Orange Democratic Movement (ODM) baada ya kutofautiana na mkuu wa chama Raila Odinga.

Wanjigi alijiunga na chama cha Safina mnamo Jumatano.

Alipokelewa kwa Safina na kiongozi wa chama na aliyekuwa mgombea urais Paul Muite.

Wanjigi alikata uhusiano na ODM mnamo Februari 26 baada ya kuchoshwa na wafuasi wa ODM alipokuwa akijaribu kuingia katika uwanja wa Kasarani kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa chama (NDC).

Akizungumza baada ya kujiunga na chama cha  Safina, Wanjigi alisema atafanikisha yote aliyopanga katika chama hicho kinachoongozwa na Muite.

"Njia yetu ya Demokrasia haitazuiliwa. Ndoto Yetu ya Ukombozi wa Kiuchumi wa Wakenya iko hai kuliko hapo awali na tutafanikisha hilo katika Chama cha Safina. Ark imeondoka kizimbani na tunakoelekea ni Urais wa Jamhuri hii kuu,” alisema Wanjigi.

Alisema atawasilisha karatasi zake za uteuzi wa kiti cha juu wakati wa NDC ya chama hicho iliyopangwa Machi 21.

Muite, aliyekuwa Mbunge wa Eneo Bunge la Kabete na wakili mkuu, alimzindua Wanjigi kama mgombeaji urais wa chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.