Polisi amdunga mkewe hadi kifo kisha kujaribu kujitoa uhai Bomet

Muhtasari

•Afisa huyo mwenye umri wa miaka 35 alimdunga mkewe ,25, mara tatu kifuani kwa kutumia uswodi.

•Polisi huyo alipatikana akiwa hali mahututi na kukimbizwa katika hospitali ya TenWek huku mwili wa mkewe ukipelekwa katika mochari ya Longisa.

Crime scene
Crime scene

Afisa mmoja wa polisi katika kituo cha Bomet anaripotiwa kumdunga mkewe hadi kifo usiku wa Jumapili kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Afisa huyo mwenye umri wa miaka 35 alimdunga mkewe ,25, mara tatu kifuani kwa kutumia uswodi. Tukio hilo lilitokea katika nyumba yao ya kupanga iliyo mtaani Bomet.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa marehemu alijaribu kutoroka baada ya mumewe kuanza kumshambulia ila hakufanikiwa.

Wanandoa hao wanaripotiwa kushiriki mabishano makali kwa muda kabla ya mzozo wao kupelekea mauaji. Baada ya kutekeleza mauaji hayo mshukiwa alijaribu kujitoa uhai kwa kujidunga tumboni kutumia uswodi huo huo ambao alitumia kuua mkewe.

Mshukiwa alipatikana akiwa hali mahututi na kukimbizwa katika hospitali ya TenWek huku mwili wa mkewe ukipelekwa katika mochari ya Longisa.

Majirani ambao walifika kwenye eneo la tukio walimuokoa mtoto mdogo ambaye aliangua kilio kikubwa baada ya vita kuzuka baina ya wazazi wake.