Mchina apatikana ameuawa katika chumba cha hoteli Nairobi

Muhtasari

•Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mwili wa Zhou Yadi ulipatikana bafuni ukiwa umefungwa kipande cha kitambaa shingoni.

•Kwingineko katika eneo la Industrial Area, raia wanne wa Uchina walishambuliwa na kuibiwa Sh800,000 na vitu vingine vya thamani.

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Polisi jijini Nairobi wnachunguza kisa cha mauaji ya Mchina mmoja ambaye alipatikana amefariki kwenye bafu la chumba chake cha hoteli katika mtaa wa Lavington..

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mwili wa Zhou Yadi ulipatikana bafuni ukiwa umefungwa kipande cha kitambaa shingoni.

Yadi alifanya kazi kama meneja katika kampuni ya ujenzi iliyokabidhiwa kazi ya kujenga barabara kuu ya Lamu-Garissa.

Alikuwa amesafiri hadi jijini Nairobi kwa kazi rasmi na alikuwa chumbani mwake wakati alishambuliwa na watu wasiojulikana. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alinyongwa.

Waliotembelea eneo la tuki walisema kulikuwa kumechafuka na kulikuwa na dalili za mapambano ambayo huenda yalisababisha mauaji.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi. Polisi waliitwa eneo la tukio mwendo wa saa nane mchana muda mrefu baada ya tukio hilo kutokea.

Mwili wa marehemu ulipelekwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Polisi walisema bado  hakuna mtu ambaye amekamatwa na bado hawajabaini sababu za mauaji hayo.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, marehemu alikuwa amepangiwa chumba chake  peke yake.

Kwingineko katika eneo la Industrial Area, raia wanne wa Uchina walishambuliwa na kuibiwa Sh800,000 na vitu vingine vya thamani.

Wahasiriwa waliambia polisi kuwa walikuwa kwenye Godown ambapo pia wanaishi na walikuwa wakichukua chakula cha jioni wao wakati genge la watu wanane lilivamia na kuwadai pesa na vitu vingine vya thamani.

Wahasiriwa wanashuku genge hilo lilifahamu uwepo wa pesa hizo ndani ya chumba chao kwani wakizidai walipokuwa waleindelea kupora jengo hilo.

Watatu kati ya wahasiriwa hao walijeruhiwa walipokuwa wakijaribu kupinga tukio la Jumapili jioni. Polisi walisema wameanzisha msako wa kuwatafuta washukiwa hao.

Polisi pia wanawasaka washukiwa waliovamia duka moja kando ya barabara ya Juja, Nairobi, na kumwibia mhudumu Sh300,000 kabla ya kutoroka.

Washukiwa hao walikuwa wamejihami kwa bastola na kufyatua risasi moja hewani huku wakitoroka.

Polisi walisema hakuna mtu aliyejeruhiwa na uhakiki wa picha za cctv zilizonaswa unaonyesha kuwa mmoja wa washambuliaji alikuwa mfanyakazi wa zamani katika kituo hicho.

Risasi iliyotumika ilipatikana kwenye eneo la tukio.