Mbunge Sudi na Kositany wajisalimisha kwa polisi

Muhtasari
  • Ripoti za vyombo vya habari zilisema kuwa Spika wa Kaunti ya Uasin Gishu David Kiplagat alikuwa katika afisi za DCI saa za asubuhi
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Mbunge wa Soy Caleb Kositany na mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi waliheshimu wito wa polisi na kujiwasilisha katika afisi za DCI za Nakuru Jumapili.

Ripoti za vyombo vya habari zilisema kuwa Spika wa Kaunti ya Uasin Gishu David Kiplagat alikuwa katika afisi za DCI saa za asubuhi.

Wawili hao kwa sasa wanahojiwa huku polisi wakijaribu kufichua ikiwa wanasiasa hao walihusika na upangaji wa kisa ambapo kinara wa chama cha ODM Raila Odinga alipigwa mawe mnamo Ijumaa, Aprili 1.

Wabunge hao walikuwa wamekanusha madai ya kuandaa visa hivyo vya machafuko, wakisema kuwa hatua ya DCI kuwatenga ni hatua ya kisiasa.

Walibainisha kuwa walikuwa tayari kuandika taarifa kwa afisi za DCI ili kuthibitisha kutokuwa na hatia katika suala hilo.

Siku ya Jumamosi, DCI iliwataja wabunge Kositany, Sudi na spika wa kaunti ya Uasin Ngishu Kiplagat kuwa wapangaji wakuu na wafadhili wa ghasia zilizomkabili kiongozi huyo wa ODM.

Walitakiwa kufika mbele ya mratibu wa mkoa siku ya Jumapili saa tatu asubuhi.

Sudi katika taarifa yake alisema hakuwepo wakati tukio hilo likitokea.