Bajeti 2022/2023 - Ugatuzi watengewa bilioni 370 huku idara ya mahakama ikipokea b. 18.9

Muhtasari

• Serikali ilitenga shilingi bilioni 313 kwa idara za usalama zikiwemo idara ya huduma kwa polisi, idara ya magereza na idara ya ulinzi.

Waziri wa Hazina Ukur Yattani akipiga picha na mkoba wa bajeti katika Jengo la Hazina Nairobi kabla ya kuelekea bungeni Alhamisi tarehe 7 Aprili 2022. Picha: WILFRED NYANGARESI
Waziri wa Hazina Ukur Yattani akipiga picha na mkoba wa bajeti katika Jengo la Hazina Nairobi kabla ya kuelekea bungeni Alhamisi tarehe 7 Aprili 2022. Picha: WILFRED NYANGARESI

Waziri wa fedha Ukur Yatani amewasilisha katika bunge la kitaifa bajeti ya jumla ya shilingi trilioni 3.3.

Katika makadirio ya bajeti yaliosomwa katika bunge siku ya Alhamisi waziri Yatani alisema kwamba kwa jumla uchumi wa taifa ulikua kwa asilimia 7.6 katika kipindi cha matumizi ya fedha cha mwaka uliopita licha ya athari za janga la Covid-19.

Katika bajeti ya mwaka huu waziri alipendekeza mgao wa shilingi bilioni 146 kwa miradi mbali mbali chini ya Agenda kuu nne za serikali (Agenda 4 Projects).

Katika juhudi za serikali kulinda sekta ya kilimo waziri anapendekeza mgao wa shilingi bilioni 2.7 kuwakinga wakulima kutokana na gharama mbali mbali za kilimo.

Sekta ya elimu ilikuwa moja wapo ya sekta ambazo serikali ilitengea kiasi kikubwa cha pesa huku waziri Ukur Yatani akitangaza kutenga jumla ya shilingi bilioni 544 kufadhili miradi mbali mbali katika sekta ya elimu.

Wakati huo huo serikali ilitenga shilingi bilioni 313 kwa idara za usalama zikiwemo idara ya huduma kwa polisi, idara ya magereza na idara ya ulinzi.

Serikali za kaunti pia zimenufaika pakubwa katika bajeti iliyosomwa na waziri Ukur Yatani huku mgao kwa serikali za kaunti ukiongezwa kwa hadi shilingi bilioni 370. Mgao huu unatarajiwa kupiga jeki na kudhibiti miradi ya ugatuzi.

Idara ya mahakama imetengewa shilingi bilioni 18.9 pekee katika makadirio ya matumizi ya pesa mwaka huu.

Kulingana na makadirio yaliyosomwa sekta ambazo zimezoa kiasi kikubwa cha pesa ni miundo msingi na kawi.

Waziri pia amependekeza kubadilishwa kwa jina la Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (Kenya Revenue Authority – KRA)  hadi Huduma ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (Kenya Revenue Service).

Kulingana na bajeti ya kitaifa kuna upungufu wa takriban shilingi bilioni 260 ambazo waziri Yatani alisema wataziba kupitia mikopo ya kimataifa.