Nairobi Expressway kuanza kutumika Jumamosi ijayo- Rais Uhuru atangaza

Muhtasari

•"Kuanzia Jumamosi, barabara ya mwendokasi itaanza kutumika ili tuendelee kujenga Nairobi na Kenya kwa ujumla." - Uhuru amesema.

Rais Uhuru Kenyatta alipozindua mbio za City marathon.
Rais Uhuru Kenyatta alipozindua mbio za City marathon.
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema Nairobi Expressway itafunguliwa kutumika na umma mnamo Mei 14.

Akizungumza siku ya Jumapili wakati wa mbio za City Marathon, Uhuru alisema barabara ya mwendokasi itakuwa wazi kwa majaribio.

"Tutaruhusu Wakenya kutumia barabara ya mwendokasi ili tuone mianya iliyopo kabla ya kuizindua rasmi," Uhuru alisema.

"Kuanzia Jumamosi, barabara ya mwendokasi itaanza kutumika ili tuendelee kujenga Nairobi na Kenya kwa ujumla." Alisema.

Barabara hiyo inatarajiwa kupunguza muda wa kusafiri jijini Nairobi na viunga vyake haswa kwa wale watakaotumia huduma ya Electronic Toll Collection (ETC)

Wenye magari wanaweza kuchagua kutumia Manual Toll Collection (MTC) au ETC mara tu watakapofika kwenye vituo vya huduma.

Mbali na marufuku ya kupiga picha, watu wanaotumia skates, watembea kwa miguu, magari ya magurudumu mawili na matatu (tuk tuks), watumia mikokoteni na baiskeli pia wamepigwa marufuku kutumia barabara hiyo ya kilomita 27.

Mnamo Aprili 17, Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) iliwataka madereva kufanya mipango ya kutumia barabara hiyp kabla ya tarehe zake za kuanza kutumika.

 

Wenye magari watahitajika kulipa hadi Sh350 kutumia barabara hiyo.

Wiki iliyopita, serikali iliongeza ada ya kutumia barabara hiyo  kwa asilimia 16, ikimaanisha kuwa madereva watalazimika kulipa zaidi ili kufikia barabara hiyo. Ada ya barabara huenda ikabadilika siku zijazo.

Barabara hiyo ya mwendokasi iliyogharimu Sh bilioni 88 ina njia 11 za kuingia katika eneo la Mlolongo, Standard Gauge Railway, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Eastern Bypass, Southern Bypass, Capital Centre, Haile Selassie Avenue, Museum Hill, Westlands na James Gichuru Road.

Katika viwango hivyo vipya, magari madogo yanayotumia barabara hiyo kutoka Mlolongo hadi James Gichuru na kutoka Westlands yatalipa Sh360 kutoka kwa Sh310 ada ya hapo awali.