Kinoti awataja washukiwa watatu wanaosakwa na Marekani kwa makosa ya mihadarati, ulanguzi wa wanyamapori

Muhtasari
  • Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya DCI, Kinoti alitoa wito kwa Wakenya kuwa waangalifu dhidi ya washukiwa ambao alisema wanajificha
Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti
Mkuu wa idara ya DCI George Kinoti

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai George Kinoti amefichua majina ya washukiwa watatu wanaosakwa na serikali ya Marekani kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na ulanguzi wa wanyamapori.

Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya DCI, Kinoti alitoa wito kwa Wakenya kuwa waangalifu dhidi ya washukiwa ambao alisema wanajificha.

"Naomba niwaombe nyote kuwa makini na wahalifu hawa wawili wanaozurura kwa uhuru. Mmoja Abdi Hussein Ahmed, Badul Abdulaziz Saleh wote ni raia wa Kenya wanasakwa Marekani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya na wanyama pori pamoja na Mansur Mohamed Sahul ambaye alikamatwa mara kadhaa kati ya Desemba 2012 na Mei 2019," alisema.

Mkuu huyo wa DCI alisema washukiwa hao walihusika katika usafirishaji, usambazaji na utoroshaji wa kilo 190 za pembe za faru, na tani 10 za meno ya tembo kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, ikiwamo Kenya ambayo walisafirisha hadi Marekani.

Kinoti alisema washukiwa hao pia walisafirisha na kusambaza kilo moja ya heroine kutoka Kenya hadi Marekani.

Mnamo Juni 14, 2019, Mahakama ya Wilaya ya Kusini ya Marekani ya New York iliwafungulia mashtaka watu hao watatu. Interpol ilitoa notisi nyekundu kuhusiana na washukiwa hao, Sahul Mansur Mohamed na Ahmed Abdi Hussein, huku hati ya kukamatwa ikitolewa kuhusiana na Saleh Badul."

Kinoti alisema Saleh Badul baadaye alikamatwa katika mpaka wa Busia na maafisa wa upelelezi wa DCI mnamo Juni 11, 2019, na kufikishwa katika mahakama ya sheria ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200 pesa taslimu.

Aliongeza mshukiwa aliagizwa kuripoti kwa wapelelezi kila baada ya wiki mbili.

"Hata hivyo, alipoachiliwa kwa dhamana, alitoweka hadi Desemba 2019 alipoonekana mara ya mwisho," Kinoti alisema.