Rais Kenyatta aitisha mkutano wa kikanda kujadili usalama DR-Congo

Muhtasari

•Uhuru alitoa wito kupelekwa kwa Kikosi cha Kudumu cha Afrika Mashariki ili kukomesha ghasia katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
•DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao hivi majuzi waliuteka mji wa mpakani Bunagana.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameitisha mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki siku ya Jumatatu kujadili amani na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na taarifa ya serikali.

Uhuru ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Jumatano alitoa wito wa kupelekwa kwa Kikosi cha Kudumu cha Afrika Mashariki ili kukomesha ghasia katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

DRC hata hivyo inapinga Rwanda kuwa sehemu ya jeshi lililopendekezwa la kikanda na imesitisha uhusiano wa pande mbili na Kigali.

Nchi hiyo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao hivi majuzi waliuteka mji wa mpakani Bunagana.

Rwanda inakanusha madai hayo.

Rais Felix Tshisekedi katika taarifa yake aliishutumu Rwanda kwa kutaka kuikalia kimabavu nchi yake ili kutumia madini yake na kuitaka Uingereza kuishinikiza Kigali kukomesha uchokozi wake.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili umeongezeka katika wiki za hivi karibuni huku maandamano ya kuipinga Rwanda yakiripotiwa mjini Kinshasa na mashariki mwa Congo.

Siku mbili zilizopita, mwanajeshi wa Congo aliwafyatulia risasi walinda usalama wa Rwanda katika kituo cha mpakani mjini Bukavu na kuwajeruhi maafisa wawili wa polisi.

Kenya ndiyo mwenyeji wa mazungumzo ya moja kwa moja ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na makundi tofauti vya waasi.

Mazungumzo hayo bado hayajazaa matokeo yoyote.