Molo: Wanafunzi wakamatwa na bhangi wakitaka kuisambaza kwa wanafunzi wenzao shuleni

Muhtasari

•“Vijana hao wenye umri wa miaka 16 na 17 walinaswa  taarifa iliyodokezwa kuwa walikuwa wamebeba bhangi" - DCI

Smoking
Image: The Star

Wanafunzi wawili wavulana kutoka shule ya upili ya Njenga Karume kaunti ndogo ya Molo walitiwa nguvuni Jumanne baada ya kupatikana na misokoto ya bhangi.

Wanafunzi hao wanaosoma katika shule hiyo kidato cha tatu wenye umri wa miaka 16 na 17 walitiwa nguvuni baada ya makachero kudokezewa kwamba walikuwa wamebeba bhangi hiyo kuelekea shuleni ambapo nia yao ilikuwa kuwasambazia wanafunzi wenzao kama chakula cha msaada.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa makachero wa DCI, mwanafunzi huyo mmoja mwenye miaka 16 ndiye alishukiwa kuwa nyuma ya njama hiyo na alikutwa na misokoto minne ya bhangi huku mwenzake wa miaka 17 akipatikana na msokoto nusu uliotumika.

“Vijana hao wenye umri wa miaka 16 na 17 walinaswa kufuatia taarifa iliyodokezwa kuwa walikuwa wamebeba dawa hiyo iliyokatazwa shuleni na walikuwa na nia ya kuisambaza kwa wanafunzi wengine. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 anayesadikiwa kuwa mpangaji mkuu alikamatwa akiwa na roli nne, huku mshirika wake akikamatwa akiwa na kipande cha msokoto huo uliotumika,” sehemu ya repoti hiyo ilisoma.

Makachero wa DCI wamehakikishia umma kwamba wamezidisha msako dhidi ya vijana wanaosambaza bhangi huku ikiafikiwa kwamba watoto wanaoenda shule ndio wamezidi kuongezeka katika biashara hiyo haramu ya kusambaza bhangi.

Maafisa hao pia waliripoti kwamba vijana hao huenda walipewa kazi ya kusambaza bhangi kwa wanafunzi wenzao na mtu mmoja ambaye ni kichwa ngumu na ambaye kwa sasa ameingia mitini.

Ripoti za matumizi ya bhangi nchini zimeongezeka mara dufu katika siku za hivi karibuni haswa kutokana na mgombea urais wa chama cha Roots, wakili msomi profesa George Wajackoyah kutangaza kwamba moja kati ya ajenda kuu za manifesto yake ni kusukuma uhalalishwaji na bhangi nchini ili kupika jeki zoezi za kulipa deni la kitaifa ambalo kwa sasa lipo zaidi ya trilioni 9 pesa za Kenya, taifa la Uchina likiwa limeongoza katika kutoa mikopo ya kufadhili miundo msingi humu nchini.