Didmus Barasa aomba dhamana huku akisubiri kukamatwa kwa madai ya mauaji

Mbunge huyo anasema ripoti kwamba alimpiga risasi Brian Olunga zinaathiri usalama wake.

Muhtasari

•Ombi hilo linakuja saa takriban masaa 20 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuamuru akamatwe.

•Barasa anasema hakuna uchunguzi wowote ambao umefanywa lakini tayari ametajwa kuwa mhusika katika mauaji.

Kimilili MP Didmus Barasa
Kimilili MP Didmus Barasa
Image: HISANI

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amehamia mahakamani akitaka kupewa dhamana hata kabla ya kukamatwa kwake kufuatia madai ya kumpiga risasi msaidizi wa mpinzani wake.

Ombi hilo linakuja saa takriban masaa 20 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuamuru akamatwe.

Barasa kupitia kwa Wakili John Khaminwa anasema hakuna uchunguzi wowote ambao umefanywa lakini tayari ametajwa kuwa mhusika katika mauaji.

Alivishtumu vyombo vya habari kwa kukashifu suala hilo.

Anasema ripoti hasi dhidi yake zinahatarisha maisha yake, ndiyo sababu anaomba mahakama impe dhamana.

“Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, marehemu alikuwa sehemu ya kikosi cha wauaji waliotumwa kutoka Nairobi na kweli aliuawa na risasi iliyopotea njia kutokana na ugomvi na washirika wake,” anasema Barasa.

Mbunge huyo anasema ripoti kwamba alimpiga risasi Brian Olunga, Agosti 9 katika Kituo cha Kupigia Kura cha Chebukwabi zinaathiri usalama wake.

Olunga alikuwa mlinzi wa Brian Khaemba.

Suala hilo bado halijasikilizwa.