Atwoli azungumzia madai kuwa amegura nchi kufuatia hofu ya matokeo ya urais

"Mtu akitumia picha yangu ya zamani nikiwa Kuala Lumpur, Malaysia, miaka mitano iliyopita," alisema

Muhtasari

•Picha hiyo ilikuwa ikienezwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa, kwa madai kwamba matokeo ya muda ya urais yalimtia hofu.

Image: HISANI

Katibu mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Francis Atwoli amepuuzilia mbali madai kuwa amesafiri nje ya Kenya.

Katika kipindi cha masaa kadhaa ambao yamepita picha inayomuonyesha akiwa katika uwanja wa ndege imekuwa ikisambazwa mitandaoni ikidaiwa kuwa amegura nchi kufuatia huku hesabu za kura za urais zikiendelea.

Kiongozi huyo mwenye ujasiri mkubwa alizamia kwenye Twitter Ijumaa jioni na kufutilia mbali habari hizo kuwa za uwongo.

"Mtu akitumia picha yangu ya zamani nikiwa Kuala Lumpur, Malaysia, miaka mitano iliyopita," alisema kupitia Twitter.

Picha hiyo ilikuwa ikienezwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa, kwa madai kwamba matokeo ya muda ya urais yalimtia hofu.

Mnamo Juni 29 wakati wa mkutano wa Azimio huko Kakamega, Atwoli aliwahimiza Waluhya kumpigia kura mgombeaji urais wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Alidai hatakuwa na amani iwapo mgombeaji wa Kenya Kwanza William Ruto atashinda uchaguzi huo.

“Ushindi wa Raila utaokoa maisha yangu kwa sababu ikiwa Ruto atashinda, sitakuwa na amani,” akasema.

Atwoli amekuwa akipinga kuwania kwa Ruto tangu 2014, akidai naibu wa rais anayeondoka hana uadilifu wa kuwa bosi mkuu wa nchi.

Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Aliyekuwa katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju walisema siku za nyuma wataondoka nchini.