CHUMA CHENU KI MOTONI

Gavana wa Meru awaonya madereva wa kaunti wanaoegesha magari vilabuni

Kawira alitaja visa vingi ambapo wafanyikazi hujiendesha kwa magari ya kaunti hadi vilabu vya usiku.

Muhtasari

•Kawira alielezea kushtushwa na mienendo ya maafisa wa kaunti wanaotumia rasilimali vibaya.

•Miongoni mwa maafisa anaotaka waripotiwe ni wafanyikazi wanaopokea hongo na kuwahangaisha wafanyabiashara huko Meru.

Gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza
Gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza
Image: HISANI

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amewaonya wafanyikazi wa kaunti dhidi ya kutumia vibaya magari waliyotengewa kazini.

Akizungumza huko Mitunguu mnamo Ijumaa, Kawira alitaja visa vingi ambapo wafanyikazi hujiendesha kwa magari ya kaunti hadi vilabu vya usiku na sehemu zingine za burudani.

“Madereva wetu wasitumie magari waliyopewa kwenda kwenye vilabu baada ya kazi,” Kawira alionya.

Gavana huyo aliahidi zawadi ya Sh10,000 kwa kila mkazi atakayefichua dereva yeyote atakayepatikana na gari la kaunti kwenye jumba la burudani.

"Kuhusu nyinyi, umma popote unapoona gari la Serikali ya Kaunti ya Meru limeegeshwa kwenye kilabu usiku, nitumie ripoti hiyo na tutakupa Sh10,000," Kawira alisema.

Kawira alielezea kushtushwa na mienendo ya maafisa wa kaunti wanaotumia rasilimali vibaya. Miongoni mwa maafisa anaotaka waripotiwe ni wafanyikazi wanaopokea hongo na kuwahangaisha wafanyabiashara huko Meru.

"Ukiripoti mwizi yeyote wa rasilimali za umma utapata Sh10,000. Nitahakikisha kila sarafu imehesabiwa," alisema.

Hatua hiyo inalenga kuziba mianya katika ukusanyaji wa mapato ya kaunti ambayo inatatiza utoaji wa huduma na kuongeza kutoaminiana.

Hapo awali, Kawira alidokeza kuunda timu ya siri ambayo itajitahidi kukomesha utoro na ufisadi.