Mbunge wa kiume wa Senegal ampiga mwenzake wa kike bungeni

Kujibu mapigo, mbunge wa kike alimrushia kiti Bwana huyo , kabla ya wabunge wengine kuingilia kati.

Muhtasari

• Chama tawala kilipoteza nafasi za wabunge wengi, hali iliyoharibiwa kwa kiasi na wasiwasi kwamba Rais Macky Sall atawania muhula wa tatu mwaka 2024.

Machafuko yalizuka katika bunge la Senegal siku ya Alhamisi baada ya mbunge mwanamume kumpiga mwenzake wa kike kichwani katika matukio ambayo yalionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni.

Shughuli za bunge zilitatizika wakati wa uwasilishaji wa bajeti, baada ya mbunge wa upinzani Massata Samb kuondoka jukwaani na kuelekea kwa Amy Ndiaye Gniby wa muungano tawala wa Benno Bokk Yakaar na kumpiga.

Katika kulipiza kisasi, Bi Gniby alimrushia kiti Bw Samb, kabla ya wabunge wengine kuingilia kati, hata hivyo machafuko hayo hayakukoma huku wabunge hao wakibadilishana mapigo na kusababisha kusitishwa kwa kikao hicho.

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa Bw Samb aliikumbusha Bunge juu ya matamshi ambayo Bi Gniby alikuwa ametoa hapo awali ambayo alisema ni "ya kukosa adabu".

Bi Gniby basi inasemekana alijibu kutoka kwenye kiti chake kwamba "hakujali". Kisha, Bw Samb alikatisha hotuba yake na kukimbilia kwake.

Mvutano umeongezeka kati ya wanasiasa wa chama tawala na wa upinzani tangu uchaguzi wa wabunge wa Julai mwaka huu ambapo chama tawala kilipoteza nafasi za wabunge wengi, hali iliyoharibiwa kwa kiasi na wasiwasi kwamba Rais Macky Sall atawania muhula wa tatu mwaka 2024.