Mwili wa mchezaji Christian Atsu wawasili Ghana baada ya kupatikana chini ya vifusi

Naibu rais wa Ghana aliahidi mazishi maalum yanayofaa kwa mwanasoka huyo.

Muhtasari

•Ndege iliyobeba mwili wake ilitua jijini Accra Jumapili jioni ambapo wanajeshi wa Ghana walisaidia kubeba jeneza lake.

•Naibu rais alizungumzia matumaini waliyokuwa nayo kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 angepatikana akiwa hai.

uliwasili Ghana Jumapili jioni.
Mwili wa Christian Atsu uliwasili Ghana Jumapili jioni.
Image: HISANI

Mwili wa mchezaji wa Hatayspor, Christian Atsu, uliwasili nchini Ghana kutoka Uturuki siku ya Jumapili jioni baada ya kupatikana Jumamosi.

Atsu alipatikana amefariki chini ya vifusi vya nyumba yake katika mji wa Hatay, nchini Uturuki takriban wiki mbili baada ya tetemeko la ardhi kukumba nchi hiyo na kusababisha majumba mengi kuporomoka.

Ndege iliyobeba mwili wake ilitua jijini Accra Jumapili jioni ambapo wanajeshi wa Ghana walisaidia kubeba jeneza lake.

Makamu wa Rais wa Ghana, Mahamudu Bawumia, alikuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kotoka kuupokea mwili huo ambapo alizungumzia matumaini waliyokuwa nayo kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 angepatikana akiwa hai.

"Tulitumaini dhidi ya matumaini, kila siku iliyopita, tuliomba na kuomba. Lakini ole wetu, alipopatikana, hakuwa hai tena," alisema.

Aliongeza "Ni msiba chungu, chungu sana!" huku akiahidi mazishi maalum kwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Jumamosi, Ajenti wa Atsu, Murat Uzunmehmet alithibitisha kuwa mwili wake ulipatikana kufuatia shughuli ya utafutaji ya zaidi ya siku 10.

Murat alisema kwamba baadhi ya vitu vya mwanasoka huyo wa miaka 31 pia vilipatikana chini ya vifusi hivyo.

Mwili wa Atsu usio na uhai ulipatikana chini ya vifusi. Hivi sasa, vitu zaidi bado vinatolewa. Simu yake pia ilipatikana,” alisema.

Ajenti Nana Sechere alifariji familia ya marehemu na kuwashukuru wote waliosaidia katika shughuli ya utafutaji.

"Mwili wa Christian Atsu umepatikana asubuhi ya leo. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote kwa maombi yao na usaidizi,” aliandika.

Raia huyo wa Ghana alitoweka baada ya tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 7.8 kutokea nchini Uturuki alfajiri ya Februari 6.

Alikuwa ameratibiwa kuondoka saa chache kabla ya tetemeko hilo, lakini meneja wa Hatayspor alisema  Mghana huyo aliamua kusalia na klabu hiyo baada ya kufunga bao la kufutia machozi katika mechi ya Februari 5 ya Super Lig.

Atsu ambaye alikuwa akichezea klabu ya Uturuki, Hatayspor kabla ya kukumbana na kifo chake cha kuhuzunisha aliwahi kuwakilisha klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza zikiwemo Chelsea, Everton na Newcastle.