Polisi wapunguza ulinzi karibu na Ikulu kufuatia malalamishi

Hatua hiyo ilitokana na maandamano ya madereva wanaotumia barabara hizo

Muhtasari

•Polisi walliondoa vizuizi walivyokuwa wameweka kwenye barabara zinazoelekea Ikulu ya Nairobi kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanywa.

•Bungei alisema Ikulu ikiwa makao muhimu, kulikuwa na haja ya ukaguzi wa mara kwa mara wa usalama karibu.

Usalama umeimarishwa karibu na Ikulu Picha: CYRUS OMBATI
Usalama umeimarishwa karibu na Ikulu Picha: CYRUS OMBATI

Alhamisi, mamlaka ya polisi iliondoa vizuizi walivyokuwa wameweka kwenye barabara zinazoelekea Ikulu ya Nairobi kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanywa na baadhi ya Wakenya kuhusu gharama ya maisha.

Hatua hiyo ilitokana na maandamano ya madereva wanaotumia barabara hizo na ufichuzi kwamba wapangaji wa maandamano hayo hawakuwa na nia ya kuvamia Ikulu kama ilivyohofiwa.

Wapangaji walisema maandamano hayo yataanzia mashinani kabla ya kuhamia hadi mjini hapo baadaye.

Baadhi ya viongozi wa Azimio walisema jukumu la kuhamasisha mikutano ya umma limechukuliwa kutoka kwa viongozi wa juu wa Azimio.

Maafisa wa kaunti wa ODM wametwikwa jukumu la kuhamasisha Wakenya kabla ya tangazo siku ya Alhamisi.

Hii ilisababisha hatua za polisi, maafisa walisema.

Afisa mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema wameondoa vizuizi hivyo lakini wakaongeza doria iwapo kutakuwa na mipango ya kufanya maandamano huko.

“Wakazi wa Nairobi wamehakikishiwa usalama wao. Tunasimamia usalama wao na tumetuma polisi ipasavyo ili kuhakikisha kuwa mambo ni sawa. Tumeondoa vizuizi kwa sasa,” Bungei alisema.

Aliongeza kuwa Ikulu ikiwa makao muhimu, kulikuwa na haja ya ukaguzi wa mara kwa mara wa usalama karibu.

Baadhi ya viongozi wa Azimio wamelalamikia kunyanyaswa na polisi katika mitaa yao na mjini.

Wengine walisema polisi walisimamia ukataji wa miti usiku wa manane katika uwanja wa Jacaranda kama sehemu ya juhudi za kuzuia umati wa watu kukutana chini yake.

Jumatano, makumi ya maafisa wa polisi waliojihami waliweka vizuizi kwenye barabara zinazoelekea Ikulu ya Nairobi kabla ya maandamano yaliyopangwa.

Polisi waliwekwa na vizuizi katika sehemu mbalimbali kwenye barabara kuu zikiwemo Barabara ya State House, State House Avenue, Processional Way na Dennis Pritt ambapo walisimama kwa muda na kuwahoji madereva.

Maafisa  walisema wakati huo walikuwa chini ya maagizo ya kutowaruhusu waendesha pikipiki kwa kuwa wanaweza kutumika kuvusha umati hadi Ikulu kwa maandamano.

Hili lilikuja hata huku kukiwa na mkanganyiko wa iwapo hatua iliyopangwa kufanywa na viongozi wa Azimio la Umoja itaendelea.

Maagizo ya siku 14 yaliyotolewa na viongozi yalimalizika Jumatano na kumekuwa na mikutano ya kupanga hatua ya watu wengi, maafisa walisema.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alisema mipango ya hatua hiyo ya halaiki imesalia mkondoni.

“Tunataka usubiri wakati. Tarehe ya mwisho ni Jumatano saa sita usiku, kwa hivyo mtatusikia Alhamisi,” alisema.

Utafsiri: Samuel Maina