Jumatatu ni siku ya kawaida ya kazi- Mudavadi atangaza huku akimkosoa Raila

Mudavadi alimtaka Raila aeleze jinsi atakavyosaidia wale watakaopoteza kazi au pesa siku hiyo.

Muhtasari

•Mudavadi amemkashifu kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuhusu tangazo lake kuwa tarehe 20 Machi ni likizo ya umma.

•Mudavadi aliwataka viongozi kujitahidi kujenga taifa linalozingatia sheria, akibainisha kuwa kuna utaratibu wa kufanya hivyo.

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023
Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023
Image: ANDREW KASUKU

Mkuu wa mawaziri, Musalia Mudavadi amemkashifu kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuhusu tangazo lake kuwa tarehe 20 Machi ni likizo ya umma.

Huku akibainisha kuwa kuna utaratibu wa jinsi likizo ya umma inavyoamuliwa na kutangazwa, Mudavadi alishangaa ni sheria gani Raila alitumia katika tangazo lake.

"Huwezi kuwa unatembea ukiwaambia watu unataka mtu afuate sheria na wewe mwenyewe unakiuka waziwazi, ukitoa matamko ya uwongo ambayo hayana msingi wa kisheria," alisema.

Mkuu wa Mawaziri alisema hatua hiyo ni mfano wa kutokujali.

Alizungumza siku ya Jumatano wakati wa mkutano na Rais William Ruto na viongozi kutoka kaunti ya Trans Nzoia katika Ikulu.

Mudavadi aliwataka viongozi kujitahidi kujenga taifa linalozingatia sheria, akibainisha kuwa kuna utaratibu wa kufanya hivyo.

Mudavadi aliweka wazi kuwa Jumatatu ni siku ya kawaida ya kazi na kumtaka Raila afafanue jinsi atakavyosaidia wale ambao watapoteza kazi au pesa siku hiyo.

Huku akitangaza likizo hiyo kinyume cha sheria siku ya Jumanne, Raila alisema ililenga kuwaruhusu wafuasi wa Azimio kusafiri ili kushiriki katika maandamano dhidi ya kile alichokitaja kuwa serikali haramu.

"Ninatangaza leo kwa jina la Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance kwamba Jumatatu tarehe 20 Machi itakuwa siku ya mapumziko," Raila alisema akiwa katika kaunti ya Siaya.

Uwezo wa kutangaza sikukuu za umma uko kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Hii ina maana kwamba wakati huu, ni Waziri Kithure Kindiki pekee anaweza kutangaza sikukuu ya umma kihalali.