Teargas ya leo ni tamu, nunua zaidi- Babu Owino amwambia Ruto

Babu aliwakashifu polisi kwa madai ya kuwaua waandamanaji watatu.

Muhtasari

•"Tunataka kuwashukuru maafisa wa polisi kwa kutumia pesa za walipa ushuru kununua vitoa machozi, kwanza ya leo ni tamu sana, mnunue zaidi," Owino alisema.

•Wabunge hao walirushiwa vitoa machozi walipokuwa wakihutubia wanahabari na wafuasi wa Azimio katika KICC.

wakati wa maandamano mnamo Machi 20, 2023.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wakati wa maandamano mnamo Machi 20, 2023.
Image: EZEKIEL AMINGA

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amewataka maafisa wa polisi kununua vitoa machozi zaidi.

Owino ni miongoni mwa viongozi wa Azimio la Umoja wanaoshiriki maandamano jijini Nairobi.

"Tunataka kuwashukuru maafisa wa polisi kwa kutumia pesa za walipa ushuru kununua vitoa machozi, kwanza ya leo ni tamu sana, mnunue zaidi," Owino alisema.

Baada ya maandamano katika KICC, viongozi hao waliwahutubia waandishi wa habari nje ya majengo ya Bunge.

Zaidi ya hayo, Babu aliwakashifu polisi kwa madai ya kumuua muandamanaji mmoja katika eneo la Jacaranda na wengine wawili katika eneo la Kibra.

Aliongeza kuwa hakuna kinachoweza kuwazuia kuendelea na maandamano.

"Leo ni mazoezi tu, tutafanya hivi kila wiki. Hatutarudi nyuma kwa sababu ya vitoa machozi na risasi," alisema.

Mbunge wa Kathiani ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Robert Mbui alisema wanawajibisha polisi kibinafsi kwa ukatili wowote wanaowafanyiwa waandamanaji.

Seneta wa Kitui Enock Wambua amesema maandamano ya leo ni mazoezi na kuongeza kuwa wanapanga zaidi katika siku na wiki zijazo..Polisi katika kujaribu kuwazuia waandamanaji walirusha vitoa machozi lakini wabunge hao wakaungana na wafuasi wengine wa Azimio walipokaribia KICC.

Wabunge hao walirushiwa vitoa machozi walipokuwa wakihutubia wanahabari na wafuasi wa Azimio katika KICC.

Baadhi ya wabunge wanaoshirikiana na upinzani wamekamatwa kwa kuongoza maandamano katikati mwa jiji.

Baadhi ya waliokamatwa ni pamoja na; Kiongozi wa Wachache katika Seneti Stewart Madzayo, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na kiongozi mwingine mmoja wa kike.