Kiambu: Mama na mwanawe wapatikana wamekufa kwenye kisima

Kulingana na wenyeji, Simon Kimani, 40, anaripotiwa kumsukuma mamake Mercy Mugure mwenye umri wa miaka 75 kwenye kisima kabla ya kujiua kwa kuruka kwenye kisima hicho.

Muhtasari

• Kikosi cha idara ya kudhibiti majanga kaunti kilifika eneo la tukio na kupata miili hiyo.

• Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti huku kamanda wa polisi  Kiambu Perminus Kioi akisema wanachunguza mkasa huo

polisi wachunguza kifo kwenye kisima Kiambu

Polisi wanachunguza kisa ambapo miili ya mama na mwanawe ilipatikana katika kisima cha familia katika kaunti ya Kiambu.

Kulingana na wenyeji, Simon Kimani, 40, anaripotiwa kumsukuma mamake Mercy Mugure mwenye umri wa miaka 75 kwenye kisima kabla ya kujiua kwa kuruka kwenye kisima hicho.

Kimani na mama yake walikuwa katika hali ya kutoelewana kuhusu kujihusisha kwake na kikundi cha kidini chenye imani na mila zenye utata.

Imani zenye utata zilizozua uhasama huo ni pamoja na kufanya Ukeketaji (FGM) na kuruhusu ndoa kwa wake wengi.

Jirani alisema mama huyo alipinga hatua yake na alikuwa amemwonya mwanawe dhidi ya kitendo hicho ambacho kilimkasirisha.

Kikosi cha idara ya kudhibiti majanga kaunti kilifika eneo la tukio na kupata miili hiyo. Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti huku kamanda wa polisi Kiambu Perminus Kioi akisema wanachunguza mkasa huo.

Katika tukio ingine, polisi katika mtaa wa Bahati Nairobi wanachunguza kifo cha ghafla cha mzee wa miaka 40 katika nyumba yake. Mwili wa mwanamume huyo ulipatikana kwenye sakafu ya nyumba yake huku damu zikitoka puani.

Haijabainika ni nini kilisababisha kifo cha mwanamume huyo ambaye alikuwa ameachwa peke yake katika nyumba hiyo mnamo Septemba 18.

Mkewe alirudi nyumbani na kukuta imefungwa kutoka ndani kabla ya kutafuta usaidizi wa wenyeji ili kuvunja mahali ambapo mwili ulipatikana umelazwa.

Polisi walifika dakika chache baadaye na kuuhamisha mwili huo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa kifo hicho.