Babake wakili 'bandia' Brian Mwenda asema mwanawe hana hatia

Babake Mwenda, Arnold Njagi alidhibitisha kuwa mwanawe alisoma katika Chuo cha sheria cha Kenya.

Muhtasari

• Babake alisema Mwenda alisomea Diploma ya sheria ya jinai,kisha baadaye akajiunga na chuo kikuu cha Strathmore mwaka wa 2017 na kuhitimu mwaka wa 2020.

• Mwaka wa 2021 ndipo alianza safari yake ya masomo ya sheria katika chuo cha sheria nchini  (Kenya School of Law) na akamaliza mwaka wa 2022 Disemba.

• Safari yake ya kuwakilisha kesi kortini ameianza Januari mwaka huu.

Babake Brian Mwenda
Babake Brian Mwenda
Image: Facebook

Babake Brian Mwenda mwanasheria ambaye anadaiwa kuhudumu bila leseni ya uwakili, Ardold Njagi anasema ana uhakika mwanawe ni wakili na kinyume na madai kuwa hajahitimu anasema  mwanawe alienda chuo cha sheria na kuhitimu.

Katika video iliyochapishwa kwenye ukursa wa Facebook,babake Mwenda alidhibitisha kuwa mwanawe alisoma katika Chuo cha sheria cha Kenya (Kenya School of Law) na kwamba yeye ni wakili ambaye amehitimu.

"Mwenda alisomea Diploma ya sheria ya jinai,kisha baadaye akajiunga na chuo kikuu cha Strathmore mwaka wa 2017 na kuhitimu mwaka wa 2020. Mwaka wa 2021 ndipo alianza safari yake ya masomo ya sheria katika chuo cha sheria nchini  (Kenya School of Law) na akamaliza mwaka wa 2022 Disemba. Safari yake ya kuwakilisha kesi kotini ameianza Januari mwaka huu," alisema.

Alieleza kuwa Brian Mwenda alianza kuwakilisha wateja kortini kwa jamaa mmoja ambaye alikuwa mtu wa familia yake.

"Ameonekana mara nyingi kwa mahakama mbali mbali akiwakilisha kesi,na hiyo ni dhibitisho kuwa amesoma,hata mimi hapa nilipo nina uhakika kuwa  amesoma na amehitimu kwa hivyo sina tashwishi na kijana wangu,alisema babake Mwenda," alisema babake. 

Alidhibitisha kuwa Mwenda anatia kila jitihada kwa kila kesi ambayo anaiwakilisha na kusema kuwa mpaka sasa wakati ambapo hali ya taaruki kuhusu kisomo chake inatanda,amefanikiwa kushinda kesi 26 mahakamani.

Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kushughulikia jambo hilo kwa haki ili kubaini ukweli wa jambo hilo.

Ripoti zinaonyesha kuwa kabla ya madai haya kujiri, Mwenda alishinda kesi 26 mbele ya Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu na Majaji wa Mahakama ya Rufaa.