Sakaja aamuru msako mkali dhidi ya wachuuzi katikati mwa jiji

Gavana wa Nairobi anasisitiza sharti sheria ifuatwe na hatabadili mawazo yake.

Muhtasari

•Gavana huyo pia alisema uchuuzi  kando ya Tom Mboya na Moi Avenue ni marufuku

•Sakaja alieleza kuwa maeneo hayo yamewekwa alama kwa ajili ya mradi wa mabilioni ambao unalenga kupunguza msongamano wa jiji

 

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya maafisa wa ukaguzi na viongozi wa wachuuzi Oktoba 25, 2023. Picha: MAUREEN KINYANJUI
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya maafisa wa ukaguzi na viongozi wa wachuuzi Oktoba 25, 2023. Picha: MAUREEN KINYANJUI

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametangaza msako mkali ambao utalenga kuwadhibiti wachuuzi katikati mwa jiji.

"Hakutakuwa na uchuuzi barabarani, ninaitekeleza  sheria hiyo kuanzia kesho (Alhamisi) asubuhi, hata karibu na kituo cha basi. Sitaruhusu hilo,” alisema.

Gavana huyo alikuwa akizungumza wakati wa kikao cha mashauriano kati ya maafisa wa utekelezaji, wachuuzi na mawaziri wa kaunti.

Sakaja alisisitiza kuwa ni lazima sheria ifuatwe katika maeneo ambayo biashara imepigwa marufuku, akisema kuwa hatabadili mawazo yake.

"Nairobi itakuwa jiji la utulivu na heshima. Hakutakuwa na uchuuzi  barabarani na hilo haliwezi kujadiliwa," alisema.

Sakaja aliongeza kuwa hatua hiyo haitakuwa tu kwa usalama wa wachuuzi wanaohatarisha maisha yao kwa kuuza bidhaa zao barabarani bali itawawezesha madereva kuendesha magari  kwa urahisi.

 Gavana huyo pia alisema uchuuzi  kando ya Tom Mboya na Moi Avenue ni marufuku, akieleza kuwa maeneo hayo yamewekwa alama kwa ajili ya mradi wa mabilioni ambao unalenga kupunguza msongamano wa jiji.

 Sakaja  pia alimwagiza Afisa Mkuu anayesimamia Usalama Anthony Kimani kuhakikisha kuwa maafisa wote wamevalia sare.

"Sitaki askari yeyote kufanya kazi bila sare isipokuwa  wale ambao ni sehemu ya operesheni kwenye kikosi cha kukabiliana na wachuuzi",aliema Sakaja.