Serikali yakiri kuchelewa kwa baadhi ya vitabu vya gredi 8

Katibu wa kudumu alisema wanafunzi wa darasa la 8 wamepata vitabu vyao vingi na kwamba ni vitabu viwili tu ambavyo havijafikishwa shuleni.

Muhtasari

• Kulingana na serikali vitabu vya wanafunzi wa gredi ya 9 vitakuwa tayari katika miezi miwili ijayo.

Belio Kipsang,Katibu wizara ya Elimu Picha:Screengrab
Belio Kipsang,Katibu wizara ya Elimu Picha:Screengrab

Click here to edit this text.Katibu wa kudumu wa Elimu ya Msingi Belio Kipsang amesema wanafunzi wa darasa la 8 CBC watakuwa na vitabu vyao vyote katika muda wa siku 30 zijazo.  

Belio alisema wanafunzi wa darasa la 8 wamepata vitabu vyao vingi na kwamba ni vitabu viwili tu ambavyo havijafikishwa shuleni. 

 "Nataka kuthibitisha kwamba vitabu vya darasa la 8 tayari viko shuleni. Tunachokamilisha ni yale maeneo mawili ya masomo yaliyofanyiwa mabadiliko," alisema. 

 "Lakini, vitabu vyote vya maeneo mengine ya kujifunzia tayari vipo shuleni na vitabu vilivyobaki vinapaswa kuwa shuleni katika siku 30 zijazo kwa maeneo ambayo yalifanyiwa mabadiliko kwa sababu tulilazimika kurejelea ili kurekebisha maeneo kwa kile kilichohitajika."

Aidha, Belio alisema tayari Wizara inaandaa vitabu kwa ajili ya wanafunzi wa gredi ya 9.  Alisema hii ni muhimu ili kuwapa walimu muda wa kutosha wa kufahamu vitabu hivyo hata kabla ya wanafunzi kufika shuleni. 

“Tunapotayarisha mtihani wa gredi ya 9, tutaweza kufanya hivyo kutokana na maudhui ambayo walimu wetu wamekuwa wakiyathamini,” alisema.  

Katibu wa kudumu alisema vitabu vya wanafunzi wa gredi ya 9 vitakuwa tayari katika miezi miwili ijayo.  Kulingana na mapendekezo ya jopo maalum la Rais kuhusu Marekebisho ya Elimu (PWPER), Taasisi ya Kenya ya Ukuzaji Mtaala (KICD) ilipunguza idadi ya masomo chini ya Mtaala unaozingatia Umahiri.  

Katika notisi ya Desemba 20, 2023, kwa wakurugenzi wa Elimu wa kanda, kaunti na kaunti ndogo, Belio alisema KICD iliamua kwa mashauriano na Wizara ya Elimu.  

PWPER ilisema maeneo ya kujifunzia chini ya CBC yanahitajika kuunganishwa ili kushughulikia mapengo na wingi wa masomo.