Maafisa wawili wakamatwa kwa kudai rushwa huko Bungoma

Maafisa hao wanadaiwa kudai hongo ili kuachilia pikipiki zilizokuwa zinazuiliwa katika kituo cha polisi kwa madai kwamba zilikuwa za wizi.

Muhtasari

• EACC ilisema afisa mwingine mshirika wa wawili hao yuko mafichoni na wamemuagiza ajiwasilishe kwa Afisi ya EACC Kanda ya Bungoma.

Pingu
Image: polisi wawili washikwa kwa madai ya hongo

Maafisa wawili wa polisi katika Kaunti ya Bungoma wamekamatwa kwa madai ya kupokea hongo.

Maafisa hao wanadaiwa kudai hongo ili kuwezesha kuachiliwa kwa pikipiki zilizokuwa zinazuiliwa katika kituo cha polisi kwa madai kwamba zilikuwa za wizi.

Akithibitisha kukamatwa kwa washukiwa, Msemaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Eric Ngumbi alisema washukiwa hao watashtakiwa chini ya Sheria ya Utoaji Hongo siku ya Jumatano.

Watafikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi mjini Bungoma.

Washukiwa hao kwa sasa wanazuiliwa katika afisi ya EACC kaunti ya Bungoma ili kushughulikiwa na baadaye watahamishwa hadi Kituo cha Polisi cha Bungoma wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Kukamatwa huko kumejiri baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma (DPP) kukubaliana na mapendekezo ya  EACC kuwafungulia mashtaka washukiwa hao.

EACC ilisema afisa mwingine mshirika wa wawili hao yuko mafichoni na wamemuagiza ajiwasilishe kwa Afisi ya EACC Kanda ya Bungoma.

Haya yanajiri siku chache baada ya Tume hiyo kumkamata afisa mmoja siku ya Ijumaa, kwa madai ya kujipatia Shilingi 30,000 kutoka kwa mlalamishi.

Afisa huyo wa kiume alifumaniwa kwenye duka la pombe.

Tume ya Kupambana na Ufisadi ilisema afisa huyo alidai kiasi hicho kutoka kwa mlalamishi ili kuwaachilia ndugu wawili aliowakamata na kuwafungia seli tangu Alhamisi bila kuwasajili kwenye Kitabu cha Matukio (OB) kama inavyohitajika.