Maafisa wa KWS wapata mabaki ya mwili wa binadamu baada ya fisi kushambulia wanafunzi wa MMU

Kulingana na taarifa ya shirika hilo familia ya marehemu ilitambulika na kujulishwa.

Muhtasari

• KWS hata hivyo imetowa wito kwa wenyeji kuchukuwa tahadhari kwa sababu eneo la Kusini mwa Mbuga ya Nairobi halina ua kwa sababu hutumika na wanyama kuhama kwenda mbuga zingine.

Fuzu la kichwa cha binadamu aliyekuwa amekuliwa na fisi lilipatikana shambani Thika
Fuzu la kichwa cha binadamu aliyekuwa amekuliwa na fisi lilipatikana shambani Thika
Image: MAKTABA

Maafisa wa shirika la wanyamapori nchini KWS siku ya Jumatatu walipata mabaki ya mwili wa binadamu katika eneo la Ole Kasasi, Rongai kaunti ya Kajiado.

Kulingana na taarifa ya shirika hilo familia ya marehemu ilitambulika na kujulishwa. Maafisa wa kitengo maalum cha usimamizi wa wanyapori waliotoroka mbuga (PAMU) walikuwa wametumwa kuwakoa wanafunzi wawili wa chuo kikuu cha Multi Media ambao walikuwa wamevamiwa na fisi katika eneo la Ole Kasasi walipopata mabaki ya binadamu.  

“La kusikitisha ni kwamba kikosi kingine cha (PAMU) kilichosalia kushika doria kiligundua sehemu ya mabaki ya binadamu kwenye eneo la tukio, ambayo yalichukuliwa na Polisi. Mabaki hayo yamethibitishwa na familia kujulishwa”, taarifa ya KWS ilieleza.

Siku ya Jumatatu saa mbili usiku wanafunzi wawili wakiume wa Chuo Kikuu cha Multi Media, walishambuliwa na kujeruhiwa vibaya na fisi katika eneo la Ole Kasasi huko Rongai, Kaunti ya Kajiado. Baada ya kupokea ripoti, KWS ilituma Kitengo cha Usimamizi wa Wanyama (PAMU), ambao waliwakimbiza wanafunzi hao katika Hospitali.  

Majeruhi walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu maalum, baada ya kupokea huduma ya Kwanza. Kisa hiki kulipelekea wanafunzi wa Chuo cha MMU kuandamana na kutoa wito kwa shirika la KWS kudumisha usalama wao kwa kukabili wanyamapori wanao randaranda na kuhatarisha maisha yao.  

 

Wakati wa oparesheni hii inayoendelea kuwasaka fisi wanao randaranda katika eneo la Ole Kasasi maafisa wa kitengo maalum cha KWS walifanikiwa kumuua fisi mmoja.

“Timu ya PAMU mara moja ilimuua fisi mmoja na kuendelea na operesheni zaidi kubaini mapango ya fisi. Wataalam wa afya ya wanyama waliondamana na kikosi cha KWS wanachunguza mzoga wa fisi aliyeuawa , ili kubaini kama anaweza kuwa ameambukizwa na maradhi ya kichaa cha mbwa au magonjwa mengine hatari.

KWS hata hivyo imetowa wito kwa wenyeji kuchukuwa tahadhari kwa sababu eneo la Kusini mwa Mbuga ya Nairobi halina ua kwa sababu hutumika na wanyama kuhama kwenda mbuga zingine.

“ KWS inatoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuwa waangalifu kwa vile sehemu ya kusini ya Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi haina uzio, na ni ukanda wa kuhama wa wanyamapori. Timu ya PAMU itasalia katika hadi fisi wote katika Ole Kasasi watakaporudishwa kwenye mbuga ili kuimarisha usalama wa wananchi,” KWS iliongeza kwenye taarifa. 

Shirika hilo lilitoa wito kwa wananchi wote kuripoti mara moja kesi zozote za dharura za wanyamapori kwa afisi iliyo karibu nao ya KWS au wawasiliane kwa nambari ya simu ya Huduma ya 24/7 kwa 0800 597 000 kwa msaada wa haraka.