Haiti yazidi kuporomoka huku magenge yakiimarisha udhibiti

Hii inatokea baada ya shambulio la kudumu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao bado umefungwa kwa safari zote za ndege.

Muhtasari

• Waziri Mkuu Ariel Henry alijaribu kurejea Haiti kutoka Marekani wiki iliyopita.

• Ndege yake ilikataliwa kutua, Pia alikataliwa kutua Jamhuri ya Dominika, jirani yake.

Image: BBC

Haiti inatumbukia kwa kasi sana katika machafuko.

Mwishoni mwa juma, ghasia katika mji mkuu wa Port-au-Prince ziliongezeka kwa mara nyingine tena. Magenge yenye silaha kali yalishambulia Ikulu na kuchoma sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mabomu ya petroli.

Hii inatokea baada ya shambulio la kudumu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao bado umefungwa kwa safari zote za ndege - ikiwa ni pamoja na moja iliyombeba Waziri Mkuu Ariel Henry.

Alijaribu kurejea Haiti kutoka Marekani wiki iliyopita, lakini ndege yake ilikataliwa kutua. Pia alikataliwa kutua Jamhuri ya Dominika, jirani yake.

Bw Henry sasa amekwama Puerto Rico, hawezi kukanyaga taifa analoongoza.

Miongoni mwa wale ambao walifaulu kuingia katika taifa hilo lililoathiriwa, hata hivyo, ni kundi la wanajeshi wa Marekani.

Kufuatia ombi kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Pentagon ilithibitisha kuwa imefanya operesheni ya, kama ilivyosema, "kuongeza usalama" wa ubalozi wa Marekani huko Port-au-Prince na kuwasafirisha kwa ndege wafanyakazi wote wasio wa lazima.

Muda mfupi baadaye, EU ilisema imewahamisha wanadiplomasia wake wote, wakikimbia taifa lililokumbwa na ghasia na linalokabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu tangu tetemeko la ardhi la 2010.

Mamilioni ya Wahaiti, hata hivyo, hawana uwezo wa kufanya hivyo. Wamenaswa, haijalishi mambo yanakuwa mabaya kiasi gani.

Ya msingi kuhusu Haiti:

  • Nchi hii inashirikishana mpaka na Jamhuri ya Dominika na inakadiriwa kuwa na wakazi milioni 11.5
  • Ina eneo la ardhi la kilomita za mraba 27,800, ambalo ni dogo kidogo kuliko Ubelgiji na karibu ukubwa sawa na jimbo la Marekani la Maryland.
  • Ukosefu wa utulivu wa miaka mingi, udikteta na majanga ya asili katika miongo ya hivi karibuni yameiacha Haiti kuwa taifa maskini zaidi katika Bara la Amerika Kaskazini.
  • Tetemeko la ardhi mwaka 2010 liliua zaidi ya watu 200,000 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na uchumi.
  • Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kiliwekwa mwaka 2004 kusaidia kuleta utulivu nchini humo na kiliondoka tu mwaka 2017.
  • Mnamo Julai 2021, Rais Jovenel Moïse aliuawa na watu wenye silaha wasiojulikana huko Port-au-Prince. Huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa, nchi hiyo inaendelea kukumbwa na machafuko na ghasia za magenge