Waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu

Kujiuzulu kwa Henry huenda kukasambaratisha makubaliono baina ya Kenya na nchi hiyo kwa lengo la kudumisha amani katika nchi hiyo.

Muhtasari

• Jaribio la Henry kurejea Haiti kutoka Marekani wiki iliyopita, lilikataliwa kutua.

• Pia alikataliwa kutua Jamhuri ya Dominika, jirani yake.

Kenya na Haiti zasaini mkataba wa kutuma maafisa 1,000 wa polisi
Image: PCS

Waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu wiki chache tu baada ya kutia saini na Kenya kuruhusu kutumwa kwa maafisa wa polisi kutoka Kenya ili kudumisha usalama nchini humo.

Nchi ya Haiti haijakuwa na amani tangu mwaka 2021 wakati rais wa nchi hiyo Jovenel Moise alipouawa. Nchi hiyo haijakuwa na uchaguzi hali ambayo imezorotesha udhabiti wa taifa hilo.

Maeneo mengi ya taifa hilo yamelwaliwa na makundi ya magenge huku juhudi za kuleta amani nchini humo zikigonga mwamba.

Mwishoni mwa juma, ghasia katika mji mkuu wa Port-au-Prince ziliongezeka kwa mara nyingine tena. Magenge yenye silaha kali yalishambulia Ikulu na kuchoma sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mabomu ya petroli.

Hii inatokea baada ya shambulio la kudumu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao bado umefungwa kwa safari zote za ndege - ikiwa ni pamoja na moja iliyombeba Waziri Mkuu Ariel Henry.

Alijaribu kurejea Haiti kutoka Marekani wiki iliyopita, lakini ndege yake ilikataliwa kutua. Pia alikataliwa kutua Jamhuri ya Dominika, jirani yake.

Henry alikuwa amekwama nchini Puerto Rico, kushindwa kuingia katika taifa ambalo alikuwa akiliongoza. .

Miongoni mwa wale ambao walifaulu kuingia katika taifa hilo lililoathiriwa, hata hivyo, ni kundi la wanajeshi wa Marekani.

Kufuatia ombi kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Pentagon ilithibitisha kuwa imefanya operesheni ya, kama ilivyosema, "kuongeza usalama" wa ubalozi wa Marekani huko Port-au-Prince na kuwasafirisha kwa ndege wafanyakazi wote wasio wa lazima.

Kujiuzulu kwa Henry huenda kukasambaratisha makubaliono baina ya Kenya na nchi hiyo kwa lengo la kudumisha amani katika nchi hiyo.