Frida Mokaya ateuliwa msajili mkuu wa idara ya mahakama

Awali Mokaya alishikilia nafasi ya Msajili wa JSC na ana uzoefu wa zaidi ya miaka 27 katika taaluma ya sheria.

Muhtasari

• Awali Mokaya alishikilia nafasi ya Msajili wa JSC, ambayo alichukua mnamo 2012 baada ya kuhudumu kama Hakimu Mkuu.

Fridah Mokaya alipofika mbele ya JSC kwa mahojiano.
Fridah Mokaya alipofika mbele ya JSC kwa mahojiano.
Image: JSC

Tume ya huduma kwa Mahakama (JSC) imemteua Frida Mokaya Boyani kuwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama.

JSC ilimteua Frida Mokaya baada ya kuwahoji jumla ya wagombeaji saba ambao walikuwa wameorodheshwa kwa nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kustaafu kwa Anne Amadi mnamo Januari 12, 2024.

Wagombea 43 waliomba nafasi hiyo iliyotangazwa, lakini ni wagombeaji 7 pekee waliofuzu kwenye orodha ya mchujo na kufika mbele ya tume ya JSC.

Awali Mokaya alishikilia nafasi ya Msajili wa JSC, ambayo alichukua mnamo 2012 baada ya kuhudumu kama Hakimu Mkuu. Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 27 katika taaluma ya sheria.

Wengine waliofika mbele ya JSC wakisaka nafasi hiyo ni pamoja na Macharia Rose Wachuka, Ouma Jack Busalile Mwimali, Wambeti Anne Ireri, Ndemo Paul Maina, Kendagor Caroline Jepyegen, na Kandet Kennedy Lenkamai.

Aliyekuwa msajili mkuu  Anne Amadi alistaafu baada ya takriban miaka kumi katika nafasi hiyo.