Mipango ya mazishi ya Brian Chira yafichuliwa; tarehe, kutazama mwili, sehemu ya kuzikwa

Chira atazikwa siku ya Jumanne, Machi 26, kamati ya maandalizi ya mazishi imefichua.

Muhtasari

•Chira atazikwa nyumbani kwa nyanyake baada ya ibada ya mazishi kufanyika katika eneo ambapo mlezi huyo amekuwa akiishi Githunguri, kaunti ya Kiambu.

•Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Mwanatiktok Brian Chira
Image: RADIO JAMBO

Mwili wa mwanatiktok Brian Chira utazikwa siku ya Jumanne, Machi 26, kamati ya maandalizi ya mazishi imefichua.

Mwanatiktok Baba Talisha, ambaye ni sehemu ya waandalizi wa mazishi amefichua kuwa mwanafunzi huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kabarak atazikwa nyumbani kwa nyanyake baada ya ibada ya mazishi kufanyika katika eneo ambapo mlezi huyo amekuwa akiishi Githunguri, kaunti ya Kiambu.

“Ibada itakuwa mahali ambapo nyanya yake amekuwa akiishi kwa sababu kuna uwanja mkubwa na watu watatoshea. Ni mahali pazuri sana, mtaona,” Baba Talisha alisema.

Alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa, kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.

Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.

“Ataenda kuzikwa mahali nyanya alitoka. Si kila mtu atakayefikia mahali hapo, labda familia ya karibu na watu wachache kama makasisi. Hao wengine watabaki hiyo pande ingine wakikula, penye tutakuwa tukifanyia mazishi,” aliongeza.

Mwanatiktok huyo iliwataarifu mashabiki na wanamitandaoni ambao watataka kuhudhuria mazishi ya Chira kupanga usafiri wao wenyewe akisema atatoa maelekezo.

Mwili wa Tiktoker Brian Chira mnamo Jumatatu, Machi 18, 2024, ulihamishwa kutoka Hifadhi ya Maiti ya City hadi Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Uchunguzi wa maiti ulifanywa kwenye mwili wa Chira kabla ya kuhamishwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha KU kwa ajili ya kuhifadhiwa kabla ya kuzikwa.

Familia, marafiki na mashbaki walikusanyika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City siku ya Jumatatu kutazama mwili wa Chira baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Brian Chira aliuawa katika ajali ya barabarani mnamo Jumamosi usiku Machi 16, 2024.

Taarifa za kifo cha Chira zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi mchana.

Kulingana na Polisi, Chira alifariki kutokana na ajali aliyohusika nayo katika eneo la Karuri.

Polisi pia walisema kuwa marehemu alikuwa kwenye baa moja eneo la Gacharage na baadaye kusababisha zogo.  Kisha alilazimishwa kutoka.

Baadaye, alichukua pikipiki hadi nyumbani kwake na kushuka kabla ya kujaribu kuvuka kwa miguu.

Lori lililokuwa likienda mwendo kasi lilimgonga na kuondoka kwa kasi. Halikusimama, mashahidi na polisi walisema. Suala hilo liko chini ya uchunguzi.

Habari za kifo chake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakimuomboleza