Maafisa kadhaa wakuu wa jeshi wahofiwa kufariki katika ajali ya chopper ya KDF

Helikopta ya Kenya Air Force Huey ilikuwa imetoka katika shule ya msingi ya eneo hilo ilipoanguka na kuwaka moto.

Muhtasari

• Walioshuhudia walisema kuwa iliwaka moto wakati wa kuanguka. 

• Makao makuu ya Idara ya Ulinzi ilisema taarifa itatolewa kuhusu tukio hilo. 

• Maafisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo kabla ya mipango ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi ili kupambana na wezi wa mifugo. 

Image: BBC NEWS

Maafisa wakuu wa jeshi ni miongoni mwa maafisa wanane wanaohofiwa kufariki baada ya chopa ya Jeshi la Ulinzi la Kenya kuanguka eneo la Elgeyo Marakwet. 

Pia ndani ya ndege hiyo kulikuwa na maafisa wengine wa nyadhifa za juu katika Wizara ya Ulinzi. 

Helikopta ya Kenya Air Force Huey ilikuwa imetoka katika shule ya msingi ya eneo hilo ilipoanguka na kuwaka moto. 

Makao makuu ya Idara ya Ulinzi ilisema taarifa itatolewa kuhusu tukio hilo. Chopa hiyo inasemekana ilikuwa imebeba watu 12 wakiwemo maafisa wa cheo cha Jenerali ilipoanguka. 

Walioshuhudia walisema kuwa iliwaka moto wakati wa kuanguka. Kulikuwa na mtu mmoja tu aliyenusurika anayeaminika kuwa mpiga picha, maafisa wengine walisema. Eneo hilo lilizingirwa mara baada ya tukio hilo. 

Maafisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo kabla ya mipango ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi ili kupambana na wezi wa mifugo. 

Awali polisi walisema maafisa watano walifariki na watatu walinusurika.