Wakati Jenerali Ogolla nusra ajiuzulu kutoka KDF

Marehemu Ogolla alieleza jinsi Luteni Jenerali mstaafu Nick Leshan alivyomshawishi kutojiuzulu.

Muhtasari

• "Mnamo 1998, nilijiuzulu kutoka kwa jeshi na kama itifaki inavyohitaji nilipelekwa kwake kwa mahojiano," alisimulia.

Marehemu Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla. Picha: KDF
Marehemu Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla. Picha: KDF

Siku chache baada ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Francis Ogolla kuzikwa, video imeibuka ikifichua jinsi alivyokaribia kujiuzulu kutoka kwa jeshi miaka 26 iliyopita.

Marehemu Ogolla alikuwa amehudhuria ibada ya ukumbusho ya marehemu kamanda mstaafu wa Jeshi la Wanahewa Luteni Jenerali Nick Leshan katika kanisa la Ridgeways Baptist jijini Nairobi mnamo Septemba 8, 2021.

Wakati akitoa heshima zake, marehemu Ogolla alieleza jinsi Leshan alivyomshawishi kutojiuzulu akimhakikishia kuwa ana sifa za kupanda kuwa kamanda wa Jeshi la Wanahewa.

"Mnamo 1998, nilijiuzulu kutoka kwa jeshi na kama itifaki inavyohitaji nilipelekwa kwake kwa mahojiano," alisimulia.

“Nilidhani mahojiano yangechukua dakika 10 ndipo asaini karatasi zangu, alizungumza na mimi kwa saa tatu na alipomaliza haya ndiyo maneno yake-Francis, una uwezo wa kuwa kamanda wa Jeshi la Anga, rudi ukafanye kazi.”

Ilikuwa wakati huo, kwamba alisema alichukua barua yake ya kujiuzulu na kurudi kazini.

Mnamo 2018, marehemu Ogolla alisema maneno ya Nishan yalitimia alipopandishwa cheo hadi Meja Jenerali na kuteuliwa kuwa kamanda wa Jeshi la Wanahewa.

Akikumbuka ushauri kutoka kwa Nishan, alisema kwamba alimtembelea nyumbani kwake Narok ili kumshukuru kwa maono na hekima yake.

“Nilikumbuka maneno yake. Niliendesha gari na mke wangu hadi Narok na tukaketi naye. Alizungumza nami tena kwa saa tatu na nilipokuwa naondoka alileta rundo la vitabu na kunipa na kusema nimefurahi umesikiliza,” alisema.

Mnamo 2021, marehemu Ogolla alipandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Majeshi, nafasi ambayo alihudumu hadi 2023 Rais William Ruto alipompandisha cheo kama Jenerali.

Marehemu Nishan alifariki katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi mnamo Septemba 3, 2021, ambapo alikuwa amelazwa kwa muda.

Alizikwa Septemba 10 nyumbani kwake Narok huku Ogolla akiwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria.

Aliacha kazi kama Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, akichukua nafasi ya Jenerali Jeremiah Kianga ambaye alichukua hatamu za jeshi mnamo 2005 na mwishowe alistaafu mnamo 2011.

Imetafsiriwa na Davis Ojiambo