Mswada wa Fedha wapita hatua ya pili licha ya maandamano

Kamati itafanya kazi kutengeneza toleo la Mswada ambalo Bunge linaweza kuzingatia na kupigia kura.

Muhtasari
  • Aidha alisema kuwa Mswada huo sasa utawasilishwa tena mbele ya Bunge zima Jumanne wiki ijayo.
Bunge la Kenya
Bunge la Kenya
Image: Twitter @NAssembly Kenya

Mswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 wenye utata umesomwa kwa Mara ya Pili Bungeni baada ya Wabunge 204 kupiga kura ya kuupitisha.

Spika Moses Wetangula, katika kikao cha upigaji kura Alhamisi jioni, alitangaza kuwa wabunge 115 walipiga kura kuupinga Mswada huo.

Spika Wetangula alitangaza zaidi kwamba hakuna mbunge aliyesusia upigaji kura.

Aidha alisema kuwa Mswada huo sasa utawasilishwa tena mbele ya Bunge zima Jumanne wiki ijayo.

Katika hatua hii, marekebisho ya Mswada yatawasilishwa, na Bunge litapigia kura kila kifungu.

Kufuatia hili, Mswada huo utasomwa mara ya Tatu, ambapo Bunge litachukua kura ya mwisho ya kuidhinisha au kuukataa.

Iwapo kuna kutokubaliana kwa Mswada au marekebisho yoyote yanayopendekezwa, itatumwa kwa kamati ya upatanishi.

Kamati itafanya kazi kutengeneza toleo la Mswada ambalo Bunge linaweza kuzingatia na kupigia kura.

Haya yanajiri katika siku iliyoshuhudia maandamano makubwa kutoka kwa vijana katika maeneo mengi nchini, wakilalamikia kwamba baadhi ya mapendekezo yaliyo kwenye mswada huo yanawakandamiza kiuchumi.

Waandamanaji ambao wengi wao ni chipukizi almaarufu Gen Z wanasema vipengele vinavyolenga kuongeza ushuru vitafanya maisha yawe magumu zaidi, wakati ambapo wananchi wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya uchumi.