Mwandamanaji mmoja afariki baada ya kupigwa risasi wakati wa maandamano

Rex Masai alipigwa risasi kwenye mapaja yake na kufariki kabla ya kufikishwa hospitalini

Muhtasari

•Mwandamanaji kwa jina Rex Masai, alipigwa risasi na kufariki papo hapo katika kisa kilichonaswa kwenye video majira ya jioni.

•Afisa asiye na nguo rasmi alinaswa akifyatua risasI

•Baadhi ya wakenya kwenye majukwaa ya mitandao wameagiza Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kumtambua afisa aliyefanya uhayawani huu na kumuadhibu ipasavyo

Picha ya mwendazake Rex Kanyike Masai
Image: HISANI

Mwanaume mwenye umri wa makamu alifariki siku ya Alhamisi kufuatia kizaazaa kilichozuka cha polisi kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji hewani.

Kulingana na ripoti, mwandamanaji kwa jina Rex Masai, alipigwa risasi na kufariki kabla ya kufikishwa hospitalini katika kisa kilichonaswa kwenye video majira ya jioni.

Kwenye video, afisa asiye na nguo rasmi alinaswa akifyatua risasi huku polisi wakijitahidi kwa udi na uvumba kudhibiti maandamano hayo. Kisa hiki kilifanyika saa moja jioni katika eneo la kati ya jiji (CBD).

Uchunguzi wa madaktari ulithibitisha kuwa mwandamanji huyo alipigwa na risasi kwenye mapaja yake. Baada ya kisa hicho, nina yake Rex alipigiwa simu na kuarifiwa ujume huu mzito, waama wahenga, uchungu wa mwana aujuaye mzazi.

Kwa kuwa ni kisa kinachohusisha mauaji, mwili wake Rex ulihamishwa hadi kituo cha kuhifadhi maiti ya City Mortuary na uchunguzi ukitarajiwa wiki hiyo.

“Nimepatana na mama yake Rex na tupo njiani kuelekea City Mortuary. Kwa kuwa ni kesi ya mauaji, polisi wametuarifu kuwa mwili wa marehemu lazima uhifadhiwe kwa chumba cha kuhifadhi maiti cha umma.”

“Baada ya uchunguzi wa maiti, tutamhamisha Rex,” alisema mtetezi wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi.

Hayo yakijiri, baadhi ya wakenya kwenye majukwaa ya mitandao wameagiza Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kumtambua afisa aliyefanya uhayawani huu na kumuadhibu ipasavyo.

Fauka ya hayo, baadhi ya wakenya wengine walighadhabishwa kwa nini maafisa wa polisi walikuwa wakitumia risasi za kweli dhidi ya waandamanaji waliokuwa watulivu bila vurugu.

“Pumzika kwa amani Rex. Inatamausha sana kumpoteza mwenzetu kwenye mikono ya afisa anayestahili kuwalinda wakenya,” alisema mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

Polisi bado wako kwenye harakati ya kuzungumza kufuatia kisa hicho. Hata hivyo, inspekta jenerali wa polisi, Japhet Koome alisistiza kuwa polisi wanatumwa kuhakikisha waandamanaji hawafiki kwenye taasisi za serikali kama vile bunge.

“Tume ya polisi haitasamehe wala kukubaliana na juhudi za waandamanaji ya kuzuru sehemu nyeti za serikali ikiwemo bunge,” Koome alimalizia.