Vijana 14 washtakiwa kwa madai kumuibia mbunge Kuria Kimani

"Tunashuku kuwa wizi na ghasia zilizofuata zilipangwa na maslahi ya kisiasa," Odingo alisema.

Muhtasari

•Odingo alithibitisha kisa hicho akisema kuwa wamefanikiwa kupata sehemu ya mali iliyoibwa na kuongeza kuwa msako bado unaendelea.

•"Uchunguzi wetu unaendelea, na tumejitolea kuwakamata wahusika wote bila kujali hali zao," aliongeza.

ya polisi
Gari ya polisi
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ndogo ya Molo wamepata mali iliyoibwa na kuwakamata watu 14 wanaohusishwa na wizi na uharibifu wa mali ya mbunge Kuria Kimani wakati wa maandamano ya vijana dhidi ya serikali wiki jana.

 Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Molo (SCPC), Timon Odingo, alithibitisha kisa hicho akisema kuwa wamefanikiwa kupata sehemu ya mali iliyoibwa na kuongeza kuwa msako bado unaendelea hadi wahusika wote watakapofikishwa mahakamani.

“Kati ya vitu vilivyopatikana ni ng’ombe wanne kati ya saba walioripotiwa kupotea, huku mmoja akiwa tayari amechinjwa. Zaidi ya hayo, vifaa mbalimbali vya nyumbani vikiwemo duveti, meza, viti, vifaa vya elektroniki na printa vimepatikana pia,” alisema.

Odingo alielezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa wanasiasa walaghai katika kuchochea vijana na kuanzisha fujo zilizosababisha wizi huo na maandamano yaliyofuata akionya zaidi kuwa hawatasalimika iwapo watapatikana wakihusika na vitendo hivyo vya uhalifu.

 "Tunashuku kuwa wizi na ghasia zilizofuata zilipangwa na maslahi ya kisiasa," Odingo alisema.

"Uchunguzi wetu unaendelea, na tumejitolea kuwakamata wahusika wote bila kujali hali zao," aliongeza.

 Hali ilizidi kuwa mbaya wakati waandamanaji kutoka Nakuru na maeneo mengine walipojiunga na maandamano hayo, na kugeuza yale ambayo hapo awali yalionekana kama maandamano ya amani kuwa uharibifu wa mali.

Alitahadharisha kukithiri kwa vurugu na uporaji huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika eneo hilo wakati wa matukio hayo.

"Tunapongeza maandamano ya awali ya amani ya Jenerali Z lakini tunajutia upenyezaji wa watu wa nje ambao ulisababisha ghasia na uharibifu wa mali," alisema Odingo.

"Yeyote atakayepatikana akipora au kushiriki katika uharibifu wa mali atachukuliwa hatua kwa ukamilifu wa sheria," alionya.

 Wakaazi wa eneo hilo wametakiwa kuendelea kuwa waangalifu na kuripoti tukio lolote linalotilia shaka kwa mamlaka na kuihakikishia jamii juhudi zinazoendelea za kuleta utulivu na kuzuia machafuko zaidi.

 Wakati uchunguzi ukiendelea, washukiwa hao 14 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayohusiana na wizi na kuharibu mali.

Urejeshaji wa mali iliyoibwa ni hatua muhimu katika kurejesha utulivu huko Molo, hata wakati polisi wanaendelea kufuatilia na kudumisha uwepo thabiti ili kuzuia kuongezeka kwa fujo.