"Mheshimu faragha yetu!" Mke wa mwanahabari aliyeuawa na polisi huko Kajiado avunja kimya

Bi Javerla pia aliwataka wanasiasa na vyombo vya habari kutofika nyumbani kwao na kamera

Muhtasari

•Arshad Sharif aliuawa kwa kupigwa risasi Jumapili usiku katika kaunti ya Kajiado, katika kile polisi walichokitaja kuwa utambulisho usio sahihi.

•Bi Javerla alimuomboleza marehemu Arshad Sharif , sio kama mumewe tu mbali pia kama rafikiye mkubwa na mwanahabari ampendaye zaidi.

Image: TWITTER// JAVERIA SIDDIQUE

Javerla Siddiqque, mke wa mwanahabari mwandamizi wa Pakistan aliyeuawa kwa kupigwa risasi Jumapili usiku kwenye barabara kuu ya Nairobi-Magadi amevunja ukimya kuhusu kifo hicho cha kuhuzunisha.

Bi Javerla alimuomboleza marehemu Arshad Sharif , sio kama mumewe tu mbali pia kama rafikiye mkubwa na mwanahabari ampendaye zaidi.

"Nimepoteza rafiki, mume na mwanahabari ninayempenda leo, kwa mujibu wa polisi, alipigwa risasi nchini Kenya," alisema kupitia Twitter.

Hata akiomboleza mume wake, mwandishi huyo alitoa wito wa faragha katika kipindi kigumu ambacho familia inapitia kwa sasa.

Alivitaka vyombo vya habari na wanamitandao kusita kusambaza picha za familia yao, maelezo ya kibinafsi na picha za mwisho za marehemu kutoka hospitalini.

"Mheshimu faragha yetu na kwa kuvunja habari tafadhali msichapishe picha zetu za familia, maelezo ya kibinafsi na picha zake za mwisho kutoka hospitali. Tukumbukeni katika maombi yenu," alisema 

Bi Javerla pia aliwataka wanasiasa na vyombo vya habari kutofika nyumbani kwao na kamera katika kipindi hiki.

"Tafadhali @Twitter ondoeni picha za mwisho za marehemu mume wangu @arsched kwenye tovuti yenu mitandao ya kijamii. Wanasiasa na vyombo vya habari havikaribishwi na kamera ndani ya nyumba yetu," alisema.

Arshad Sharif aliuawa kwa kupigwa risasi Jumapili usiku katika kaunti ya Kajiado, katika kile polisi walichokitaja kuwa utambulisho usio sahihi.

Marehemu alipigwa risasi kichwani na kuuawa na polisi baada ya yeye na dereva wake kudaiwa kukiuka kizuizi cha barabarani kilichokuwa kimewekwa kuangalia magari yanayotumia barabara kuu ya Nairobi-Magadi.

"Walikuwa wakiendesha gari kutoka mji wa Magadi kuelekea Nairobi walipotakiwa kusimama kwenye kizuizi cha barabarani kilichokuwa na kundi la maafisa wa polisi," polisi walisema.

Makao makuu ya polisi yalisema Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi itasimamia kesi hiyo.

Afisa mkuu wa polisi alithibitisha kupigwa risasi kwa marehemu na kuongeza taarifa ya kina itatolewa baadaye.

"Tulikuwa na tukio la kupigwa risasi ambalo liligeuka kuwa kisa cha utambulisho kimakosa kilichohusisha mwandishi wa habari. Tutatoa taarifa zaidi baadaye,” afisa huyo alisema.

Kulingana na polisi, katika kizuizi hicho cha barabarani, kulikuwa na mwito kwa polisi kulizuia gari sawa na walilokuwa wakiendesha kufuatia tukio la utekaji nyara eneo la Pangani, Nairobi ambapo mtoto alitekwa nyara.

Na dakika chache baadaye, gari la Sharif lilijitokeza kwenye kizuizi cha barabara na wakasimamishwa na kutakiwa kujitambulisha.

Inadaiwa walishindwa kusimama na kupita kwenye kizuizi cha barabarani.

Hii ilisababisha kufukuzwa na kupigwa risasi kwa muda mfupi na kumwacha Sharif akiwa amefariki.  Gari lao lilibingirika na dereva wake alijeruhiwa na kupelekwa hospitali.

Baadaye aliwaambia polisi yeye na mwenzake aliyeuawa walikuwa wanahabari na walikuwa wakielekea eneo la Magadi.

Habari za tukio hilo zilisambaa kwa kasi nchini Pakistan ambapo mwandishi huyo wa habari alikuwa maarufu.