Mwanamke afariki na mwili kutupwa baada ya mumewe kudaiwa kulipa madaktari tapeli kutoa mimba yake

Washukiwa wanazuiliwa na wanatayarishwa kujibu mashtaka ya mauaji.

Muhtasari

•Wapelelezi walipata mwili wa mwanamke mwenye umri wa makamo katika barabara ya Outering mnamo siku ya kuamkia mwaka mpya kabla ya kuanzisha uchunguzi.

•Baadae, wapelelezi walipata taarifa kwamba mwili huo ulitupwa baada ya utaratibu wa kuavya mimba usiofanikiwa.

Image: MAKTABA

Polisi jijini Nairobi wanawazuilia washukiwa watatu kwa madai ya kuhusika katika jaribio la kutoa mimba lililosababisha kifo cha mwanamke mmoja.

Richard Onyango ambaye ni mume wa mwanamke aliyefariki wakati akifanyiwa utaratibu huo haramu anadaiwa kusaidia kutafuta huduma za madaktari wawili wanaoshukiwa kuwa tapeli ili kuutoa ujauzito ambao mkewe alikuwa amebeba.

Kulingana na DCI, wapelelezi ambao wanafanya kazi katika eneo la Starehe walipata mwili wa mwanamke mwenye umri wa makamo katika barabara ya Outering mnamo siku ya kuamkia mwaka mpya kabla ya kuanzisha uchunguzi.

"Mwili huo uliokuwa umefungwa kwenye shuka nyeupe uligunduliwa ukiwa umetupwa kwenye mtaro wa maji ya mvua karibu na kituo cha mafuta cha Shell, kando ya barabara hiyo yenye shughuli nyingi, huku matokeo ya awali yakionyesha huenda aliuawa kwingine na mwili kutupwa eneo hilo na watu wasiojulikana," taarifa ya DCI ilisoma.

Baadae, wapelelezi walipata taarifa kwamba mwili huo ulitupwa baada ya utaratibu wa kuavya mimba usiofanikiwa ambao kulingana na DCI ulifanyiwa na daktari Richard Orambo anayemiliki kituo cha afya cha Watergate, eneo la Mathare Area 1.

Orambo anadaiwa kushirikiana na daktari Francis Messo wa kliniki ya Busanzi iliyo Dandora Phase 4 na wakati waliposhindwa kuendelea na utaratibu huo, wanaripotiwa kumkimbiza kwenye zahanati nyingine haramu iliyo Kiambu.

"Ni walipokuwa njiani kuelekea Kiambu ambapo mgonjwa alipoteza maisha na watatu hao wakatupa mwili wake kwenye mtaro wa maji ya dhoruba ili kuficha ukweli. Maafisa wa upelelezi wamewakamata wahudumu hao wawili na mume wa marehemu ambaye alitambulishwa kama Richard Onyango ambaye alifanya malipo ya zoezi hilo lililoshindikana," kitengo cha DCI kimeripoti.

Washukiwa hao watatu kwa sasa wanazuiliwa na wanatayarishwa kujibu mashtaka ya mauaji.