"Sijui kwa nini niko hapa, Yesu atanisaida" MacKenzie azungumza baada ya kufikishwa mahakamani

MacKenzie aliweka wazi kwamba hafahamu chochote kinachoendelea katika shamba lake la Shakahola.

Muhtasari

•Akiwa mahakamani, MacKenzie alizungumza na wanahabari ambapo alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi kesi hiyo inavyoendelea.

•MacKenzie alibainisha kuwa anaamini Mungu wake atampigania na hatimaye ataibuka mshindi katika kesi inayomkabili.

katika mahakama ya Shanzu mnamo Juni 2, 2023
Mchungaji Paul MacKenzie katika mahakama ya Shanzu mnamo Juni 2, 2023
Image: SCREENSHOOT

Mchungaji wa Malindi mwenye utata Paul MacKenzie aliwasilishwa mbele ya Mahakama ya Shanzu siku ya Ijumaa ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha ombi aendelee kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi.

Akiwa mahakamani, MacKenzie alizungumza na wanahabari ambapo alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi kesi hiyo inavyoendelea.

"Kwa kweli ata sioni maendeleo. Ata sijui kwa nini niko hapa mwanzo. Wacha tusubiri tuone," MacKenzie alisema.

Mwanzilishi huyo wa kanisa la Good News International alilalamika kuwa mambo yanavyokwenda anahisi kudhulumika.

"Sijaona lolote limeniweka hapa. Nasubiri nisikie," alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa anaamini Mungu wake atampigania na hatimaye ataibuka mshindi katika kesi inayomkabili.

"Najua Yesu wangu ninayemtumikia na ninayemuamini atanisaidia," alisema.

MacKenzie aliweka wazi kwamba hana ufahamu wa chochote kinachoendelea katika shamba la Shakahola ambako baadhi ya wafuasi wake wanadaiwa kuzikwa.

Alibainisha kuwa amekuwa chini ya ulinzi wa polisi kwa miezi mawili hivyo hajapata nafasi ya kufuatilia yanayoendelea.

Alipoulizwa anayopitia rumande alisema, "Kwa kweli singetaka nizungumzie hayo kwa vyombo vya habari. Nafikiri kidogo yanahitaji muda wake."

Katika ombi la kutaka kuongezewa muda, upande wa mashtaka unasema  bado haujahitimisha uchunguzi na wanahitaji muda zaidi.

"Kurudishwa rumande kwa muda wa siku 60 ni muda mdogo zaidi unaowezekana ambao upelelezi unaweza kukamilika chini ya mazingira yaliyopo na ni njia ndogo zaidi za kudumisha Uadilifu wa upelelezi dhaifu," zilisomeka karatasi za mahakama.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa hakuna mabadiliko ya hali ya kuachiliwa huru kwa Mackenzie pamoja na washukiwa wengine 17 tangu uamuzi wa mahakama hiyo mnamo  Mei 10 wakati waliporudishwa rumande.

"Bado kuna sababu za msingi za kuwanyima dhamana hadi upelelezi ukamilike na kuna uwezekano mkubwa wa mashtaka makubwa dhidi ya washukiwa," zinasomeka karatasi  za mahakama.

Kufikia sasa miili ya watu zaidi ya 243 imeshafanyiwa upasuaji katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi katika Kaunti ya Kilifi.