Watu 6 wateketea hadi kufa baada ya magari mawili kugongana Machakos

Muhtasari

•Matatu ya abiria 14 iligongana uso kwa uso na gari la kibinafsi karibu na daraja la Kwamajini Ijumaa asubuhi.

•Walioshuhudia walisema moto  ulizuka baada mtungi wa gesi kulipuka wakati magari hayo yaligongana.

Watu 6 wamefariki kufuatia ajali ya barabarani Machakos
Watu 6 wamefariki kufuatia ajali ya barabarani Machakos
Image: GEORGE OWITI

Watu sita wamefariki huku wengine nane wakipata majeraha kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Yatta, kaunti ya Machakos. 

Chanzo cha polisi kilisema kuwa ajali hiyo kilitokea baada ya matatu ya abiria 14 kugongana uso kwa uso na gari la kibinafsi karibu na daraja la Kwamajini Ijumaa asubuhi.

Chanzo hicho kilisema majeruhi wanane walikimbizwa katika hospitali ya Matuu Level 4 wakiwa na majeraha mabaya ya moto.

 Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Yatta Jane Makau alithibitisha kisa hicho lakini hakutoa maelezo zaidi.

Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Machakos, Issa Mohamed alisema watu wanane ambao walichomeka kutokana na ajali hiyo waliondolewa katika eneo la tukio kwa ajili ya  matibabu na walikuwa na majeraha mabaya.

Alisema polisi wanachunguza tukio hilo. "Ni bahati mbaya tumepoteza abiria sita."

 Mgongano huo ulisababisha moto ambao uliwanasa waliokuwa wakijaribu kuondoka na kutatiza shughuli ya uokoaji,” alisema.