"Wewe ni kitu bora zaidi kuwahi kunifanyikia maishani" Raila amsherehekea Ida kwa ujumbe mtamu

Hivi leo Ida Odinga ametimiza umri wa miaka 72.

Muhtasari

•Mke huyo wa mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Amollo Odinga anasherehekea kutimiza miaka 72.

•Raila alimtaja mkewe kama mtu shupavu, mstahimilivu, mwenye busara na muombaji.

Picha ya kumbukukumbu ya kinara wa ODM Raila Odinga na mke wake Ida Odinga.
Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Hivi leo, Agosti 24, Bi Ida Betty Odinga anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Mke huyo wa mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Amollo Odinga anasherehekea kutimiza miaka 72.

Wakenya wa tabaka mbalimbali wameendelea kumtakia Bi Ida kheri ya siku ya kuzaliwa na kumuombea baraka maishani.

Raila mwenyewe haajachwa nyuma katika kumwandikia mkewe ujumbe wa siku ya kuzaliwa huku akimsherehekea kwa jukumu ambalo amecheza katika maisha yake.

"Katika kila siku ya kusherehekea kuzaliwa kwako kama leo, ninatafakari jinsi kwa kiwango kikubwa wewe ni kitu bora zaidi kuwahi kunitokea maishani," Raila alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Alimtaja mkewe kama mtu shupavu, mstahimilivu, mwenye busara na muombaji na kubainisha kuwa sifa hizo zake ndizo zilizofikisha familia yao ilipo.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa mke wangu mpendwa Ida Betty," Alisema.

Mwanawe Ida, Raila Juniour pia alimsherehekea kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Juniour alisema kuwa mamake amemfunza upendo mkubwa na upole na kutoa shukran kubwa kwake kwa hilo.

"Nimebarikiwa sana kuwa na mwanamke kama wewe katika maisha yangu. Umenionyesha upendo mkuu na upole kwa miaka yote na ninakushukuru sana kwa hilo. Heri ya Kuzaliwa kwako leo, mama," Alisema Raila Juniour.

Wanamitandao wengine wakiwemo wanasiasa na watu mashuhuri pia walitumia fursa hiyo kumsherehekea Ida.