Hasira ni Hasara: Mwanamke akamatwa Kayole kwa kuwaua watoto wake 2

Mwanamke mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa mtaani Kayole kwa kuwadunga kisu na kuwaua  watoto wake wawili baada ya mzozo wa kinyumbani.

Winfred Nduku  baadaye alijaribu kujiua  kwa kujidunga kisu tumboni lakini majirani walifaulu kumuokoa. Polisi na majirani wanasema mshukiwa alirejea nyumbani  usiku na kisha kuanza kugombana na mamake kuhusu kuwalisha watoto hao. Kwa sababu ya hasira  alichukua kisu na kuwadunga watoto  wake wawili walio na umri wa miaka miwili na saba. Polisi waliipata miili ya  Amina Nduku na Jamil Kilonzo ikiwa imelowa damu .

Walipelekwa katika hospitali iliyo karibu  ambako walitangazwa kuaga dunia. Mama yao alikimbizwa katika hospitali ya mama Lucy na kulazwa, hali yake ikiwa thabiti. Nyanya ya watoto hao amesema yeye na binti yake walikuwa wakigombana kuhusu chakula cha watoto hao. Mkuu wa polisi Nairobi Philip Ndolo amesema polisi wanamngoja  Nduku apone kabla ya kumhoji kwa lengo la kumshtaki kwa mauaji .