Hivi sasa! Kamati ya kutatua mzozo wa vyama yasitisha makubaliano ya Jubilee na KANU

Kamati kuu ya kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa nchini yaani 'Political Parties Disputes Resolution Tribunal' imesimamisha makubaliano baina ya chama tawala cha Jubilee na Kanu yaliyaofikiwa hiyo jana.

Kumekuwepo na gumzo baada ya rais Kenyatta kufanyia mabadiliko chama chake na kumteua Samuel Poghisio kama kiongozi wa Wengi kwenye bunge la Seneti huku Fatuma Dullo akiwa naibuye.

'Hata hivyo, uteuzi huo ulipokea pingamizi saa chache tu kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama hicho akiwemo seneta Kipchuma Murkomen na Susan Kihika walioapa kuwa watawasilisha malalamishi yao mbele ya spika na kamati hiyo.

Hatua ya kufanyia mabadiliko uongozi wa Jubilee ilidaiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha uhusiano baina ya chama hicho na kile cha Kanu, japo akitoa hisia zake hiyo jana, Kipchumba alihoji kuwa maseneta waliohudhuria mkutano huo katika Ikulu jijini Nairobi walikuwa wachache na hivyo uteuzi huo haustahiki kamwe.

Wachanganuzi wa kisiasa kwa upande wao nao wamehoji huenda rais Kenyatta ameanza kuonyesha azma ya kuanza kumtafuta mridhi wake mwingine na ambaye wamesema huenda akawa kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi.