Je! nini kilimuua jaji James Otieno Odek?

ODEK 1
ODEK 1
Jaji wa mahakama ya rufaa James Otieno Odek jana alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake Kisumu.

Jaji huyo mwenye umri wa miaka 53 alipatwa akiwa amelala chali kitandani mwake huku akiwa amejifunika blanketi hadi kifuani. Tembe tatu za kusisimua hisia ndani ya paketi ya tembe sita, zilikuwa tayari zimetumika lakini haijulikani zilitumiwa na nani, ripoti ya polisi iliyofikia gazeti la The Star ilieleza.

Odek alikuwa amelala mkono wake mmoja ukiwa nyuma. Damu ilikuwa ikitoka katika sehemu zake za siri na katika sikio la kushoto na mkono wake mmoja ulikuwa pia umekwaruzwa, mmoja wa polisi waliovunja na kuingia katika nyumba yake alisema. Nyumba yake ilikuwa imefungwa kutoka ndani.

Jaji huyo aliishi pekee yake katika mtaa wa Groovehut Apartments, mita chache kutoka kituo cha polisi cha Central mjini Kisumu. Alikuwa amewasili mjini Kisumu siku ya Alhamisi akiwa miongoni mwa jopo la majaji wa mahakama ya rufaa waliokuwa wasikize kesi magharibi mwa Kenya.

Dereva wake alimpeleka katika mtaa huo na kuondoka. Nyumba ilikuwa imefungwa kutoka ndani huku funguo na simu zake tatu zikiwa ndani. Televisheni ilikuwa haijazimwa.

Kamanda wa polisi wa kanda ya Kisumu Vincent Makokha alithibitisha kwamba Jaji Odek alipatikana asubuhi akiwa tayari amefariki baada ya polisi kuvunja nyumba yake.

Makokha alisema wachunguzi na mwanapatholojia walizuru eneo la mkasa kabla ya mwili kupelekwa kwa chumba cha maiti cha hospitali ya Aga Khan kufanyiwa upasuaji.

“Nimetuma maafisa kubaini tukio hilo kabla ya mwili kuondolewa na kupelekwa katika hifadhi ya maiti,” Aliambia the Star kwa simu.

"Dereva wake alipofika kumchunkuwa asubuhi alipata mlango umefungwa. Aliripoti kwa kituo cha polisi cha Central. Polisi walilazimika kuvunja mlango," hakimu mkuu wa Kisumu Julius Ng’arng’ar alisema.

Alisema jaji huyo alikuwa na mazoea ya kufika kazini kwa wakati na kawaida huwa amekiti katika dawati lake kabla ya saa mbili kila asubuhi. Bado haijabainika kama kifo chake kilitokana na vidonge vya kusisimua hisia, maradhi au ugonjwa au huenda alipangiwa njama.

Kukwaruzwa mkononi kulikuwa kumeashiria makabiliano lakini polisi walisema hapakuwepo ishara yoyote ya makabiliano ndani ya nyumba yake.