Je, Uhuru na Raila wanapanga kumuunga mkono Mukhisa Kituyi kuwania urais 2022?

mukhisa
mukhisa
Mukhisa Kituyi  huenda akawa mgombeaji  wa siri wa urais ambaye rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wanapanga kumuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka wa 2022, kwa mujibu wa washirika wa karibu wa viongozi hao wawili .

Wameliambia gazeti la The Star kwamba waziri huyo wa zamani wa biashara  anazingatiwa kwa nafasi hiyo endapo Odinga hatogombea  urais kwa mara nyingine.

Kuna uwezekano wa odinga kujitosa tena ulingoni kwa mara ya nne lakini hajathibitisha hilo. Inafahamika kwamba rais Uhuru Kenyatta  anamzingatia Kituyi kama  mtu anayeweza kumrithi  kwa sababu ya uzoefu wake kisiasa na  hadhi yake ya kimataifa.

Uhuru  pia anaripotiwa kumzingatia kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi kama anayeweza kumrithi. Kituyi kwa sasa ni katibu   mkuu  wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu biashara na maendeleo  (Unctad)  na kipindi chake cha kuhudumu kitamalizika Julai mwaka  wa 2021.

Malumbano katika chama cha Ford Kenya yamehusishwa na  kurejea kwake ili kuchukua usukani kabla ya uchaguzi.