Kizungu Mkuti:Wabunge wanafaa kuwa mawaziri?

Bendera
Bendera
Wabunge wamekuwa wakishinikiza kurekebishwa kwa sheria ilia kumwezesha rais kuwateua wabunge kuwa mawaziri . Katiba mpya iliyopitishwa na wakenya iliwazuia wabunge kuteuliwa  kuwa mawaziri lakini sasa pendekezo hilo limeanza kuungwa mkono . Aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura   ni wa hivi punde kuunga mkono pendekezo hilo  akisema kutowatumia wabunge kama mawaziri wa  serikali ni jambo ambalo limezua uhasama kati ya viongozi wa kisiasa na wale wa utawala wa serikali .

Dhamira kubwa ya kuwateua watalaam kuhudumu kama  mawaziri  ilikuwa kuhakikisha kwamba  wanatekeleza majukumu yao kikamilifu bila muingilio wa kisiasa lakini hilo limekosa  kuzaa matunda kwani  utendakazi wa mawaziri  watalaam haujaweza kuisadia serikali kuboresha   utoaji wa huduma kwa wananchi . Wadadisi pia wanaamini kwamba hatua  kuwanyima wabunge fursa ya kuwa mawaziri ndio hatua inayofaa kulaumiwa kwa hamu  yao ya kutaka kuongezwa mishahara na kujiongeza marupurupu kila mara.

Wanaounga mkono hatua ya kuwateua wabunge kuwa mawaziri wamesema hatua hiyo itaiwezesha serikali kuokoa fedha kwani haitawalipa mawaziri  na wabunge ila mbunge anayeteuliwa kuwa waziri ataongezwa takriban  shilingi  laki nne  kwa mshahara wake wa sasa kama mjumbe .Pia wanasema pesa zinazotumiwa kuwalipa  wafanyikazi wa mawaziri wa sasa ,magari na marupurupu zitaweza kuokolewa  endapo wabunge wataweza kuteuliwa kuwa mawaziri . Je unaunga mkono pendekezo la kuwateua  wabunge kuwa mawaziri?