Jitihada za Rais Kenyatta kumaliza FGM yapongezwa na makamu wa Rais wa Liberia

rais
rais
Makamu wa Rais wa nchi ya Liberia Jewel Taylor amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuendesha kampeni ya kumaliza ukeketaji wa wanawake nchini Kenya.

Taylor amempongeza Uhuru kwa kuwahamasisha viongozi pamoja na wazee kujitolea kumaliza FGM ifikapo 2022.

 Rais Kenyatta alikutana na viongozi wa kidini wiki iliyopita kutoka kaunti 22 ambao walisaini tamko la kuondoa FGM ifikapo 2022.

Makamu wa rais huyo wa nchi ya Liberia ambaye yuko nchini kuhudhuria mkutano wa ICPD25, alinena yote hayo siku ya alhamisi wakati alipomtembelea Rais Kenyatta kwenye ikulu.

Rais Kenyatta alionyesha matumaini kuwa juhudi zinazoendelea za kuzuia FGM zitafanikiwa.

Wawili hao pia walijadili shida ya ukosefu wa ajira katika bara hili na njia za kuimaliza.

Makamu huyo alimshukuru Rais Kenyatta kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa ICPD25, akisema kuwa mkutano huo ulimpa fursa ya kutembelea kiwanda cha shanga kule Karen ambapo wanawake wa eneo hilo hutengeneza shanga za mikono na mapambo mengine na kuyauza ili angalau wapate fedha.