Jitokezeni kwa ukaguzi wa saratani ya nyungu ya uzazi - Margaret Kenyatta

Mama wa Margaret Kenyatta ametoa wito kwa wanawake na wasichana kujitokeza kwa ukaguzi wa saratani ya nyumba ya uzazi huku ulimwengu ukiadhimisha mwezi wa maradhi ya saratani ya nyumba ya uzazi.

Mama wa Taifa alisema saratani ya nyumba ya uzazi imekuwa hoja kubwa ya afya inayoathiri familia nyingi kutokana na madhara makubwa ya kijamii na kifedha.

 “Januari ni mwezi ambapo kote ulimwenguni pamoja na taifa tunaimarisha juhudi zetu za kumaliza saratani ya nyumba ya uzazi- hiki ni chanzo kikuu cha saratani inayoathiri wanawake wetu nchini Kenya,” kasema Mama wa Taifa alipozindua kambi ya siku tatu ya matibabu bila malipo katika bustani ya Uhuru Jijini Nairobi.

Alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi ili kunufaika kutokana na huduma  za ukaguzi zisizo za malipo kwa lengo la kuzuia na kutambuliwa mapema kwa maradhi hayo.

Kambi hiyo ni ya 5 kwenye msururu unaoendelea wa shirika la Beyond Zero wa kupeleka huduma za matibabu nyanjani ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Nairobi na kufanikishwa na hatua ya mashirika 15 ya kutoa huduma mbali mbali za matibabu bila malipo.

Kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kitaifa kuafikia lengo la Shirika la Afya Ulimwenguni la kumaliza maambukizi ya virusi vya HIV na kisonono kutoka kwa mama hadi mtoto, Mama wa Taifa aliongoza Kaunti ya Nairobi kuzindua mpango wa kibiashara wa kidijitali wa kutimiza harakati hizo.

 Aidha Mama wa Taifa alitangaza juhudi za kuanzisha mpango unaojulikana kama “Tulinde Kizazi Jijini” kuongoza Kaunti ya Nairobi katika utoaji wa huduma za afya.

“Ningependa kuhimiza Kaunti ya Nairobi kujitokeza kuekeza rasilimali kwa lengo la pamoja la kumaliza maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi kutoka kwa mama hadi mtoto,” Mama wa Taifa alisema haya  huku akiongeza kwamba safari za kupeleka huduma za matibabu mashinani za shirika la Beyond Zero zimesaidia kupunguza mzigo wa afya kwa maelfu ya familia kote nchini.

“Tayari tumekuwa Narok, Pokot Magharibi, Kisumu na Nyandarua na sasa tuko Nairobi kuhudumia idadi kubwa ya watu inayohitaji huduma za afya,” kasema Mama wa Taifa.

Uzinduzi huo wa safari za matibabu ulitanguliwa na ziara ya Mama wa Taifa katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki ambapo alitembela wagonjwa wanaougua nasuri na wanaendelea kufanyiwa upasuaji kwa lengo la kuwarudishia hadhi huku akiwapa bidhaa za kuwasaidia.

 Tangu siku ya Jumamosi, hospitali ya Mama Lucy Kibaki ikishirikiana na Wakfu wa Utafiti wa Matibabu barani Afrika (AMREF) imekuwa ikiwafanyia upasuaji kurekebisha hali yao wale wanougua nasuri yaani fistula.

 Kufikia leo akina mama wapatao 17 walifanyiwa upasuaji wa marekebisho kushughulikia nasuri katika hospitali hiyo huku ikitarajia kwamba hospitali hiyo itawahudumia akina mama 50 ifikapo mwisho wa kambi hiyo ya matibabu. Katika hospitali hiyo, Mama wa Taifa  alifungua rasmi wadi ya kuwashughulikia watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati wao.

Waliohutubu ambao walijumuisha Waziri anayeondoka wa Afya Sicily Kariuki na balozi wa China nchini Kenya Wu Peng walimpongeza Mama wa Taifa kwa kutetea utoaji huduma bora za afya kwa wasiojiweza katika jamii kupitia kazi zake za uhisani.

“kazi ambayo umefanya inachangia kwa msingi wa mpango wa utoaji huduma za afya kwa wote,” kasema waziri Kariuki.

Balozi wa China nchini Wu Peng alisema Mama wa Taifa amedhihirisha ukakamavu na uthabiti katika kutoa huduma za afya kwa wale wasiobahatika katika jamii.

Alitoa hakikisho kwamba serikali ya China itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Kenya katika jitihada zake za maendeleo hasa nia yake ya kutimiza nguzo nne za ajenda kuu ya maendeleo.

Wengine waliohutubu ni pamoja na  Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi, Waziri wa Afya wa kaunti ya Nairobi Vesca Kangogo na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick  Amoth miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini.