KATANUKA! Magavana wa pwani sasa wasema Mkutano wa BBI utakuwa wa ‘Wapwani’.

JOHO
JOHO
 Kinanukia kivumbi jumamosi hii   katika mkutano wa BBI unaotarajiwa kufanywa huko Mombasa baada ya viongozi wa Pwani kusema kwamba  viongozi kutoka  maeneo mengine hawataruhusiwa kuzungumza wakati wa hafla hiyo bali viongozi wa Pwani pekee.

Magavana  Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Dhadho Godhana (Tana River)  na Granton Samboja (Taita Taveta)  wamesema mkutano wa jumamosi katika uwanja wa Tononoka utakuwa tu wa ‘wapwani’.

Tangazo hilo sasa huenda likazua malumbano na wafuasi wa mrengo wa tanga tanga ambao wametangaza kwamba watahuduria mkutano huo baada ya kuachwa nje katika maandalizi ya mikutano miwili ya BBI iliyofanyika Kakamega na Kisii.

" Hii ni fursa nzuri kwa watu wa Pwani kuzungumzia na kusuluhisha matatizo yao. Wengine wanafaa kungoja nafasi yao katika sehemu zao," amesema gavana wa Kilifi Amason Kingi .

Taarifa hiyo ni kinyume cha  msimamo wa Jumatano wa gavana Joho  ambaye alisema kwamba viongozi wa maeneo mengine ya nchi wana uhuru wa kuhudhuria mkutano huo wa Tononoka.

"Huwezi kwenda katika nyumba ya mtu, kisha ukaingia jikoni kujipakulia chakula," amesema Gavana Samboja .

Gavana huyo wa Taita Taveta amesema kualikwa katika mkutano hakumaanishi kwamba umepewa ruhusa ya kuzungumza. Godhana amesema watu wa Pwani wanayataka masuala yao yaweze kushughulikiwa na BBI bila kuingiliwa na masuala ya watu wa  nje.

" Asije mtu yeyote hapa kuvuruga mkutano wetu  ambao ni wa wapwani," alisema Godhana.

Magavana hao wamesema wote sita kutoka Pwani wakiwemo Fahim Twaha wa Lamu na Salim Mvurya wa Kwale wanaiunga mkono ripoti ya BBI. Wawili hao hata hivyo hawakuhudhuria kikao na waandishi wa habari katika uwanja wa Tononoka .