Kenya, Jamaica zajitolea kuthibiti zaidi uhusiano wa kibiashara

jamaica
jamaica
Kenya na Jamaica zimeahidi kuimarisha zaidi uhusiano kati yao na miongoni mwa raia wao kwa manufaa ya mataifa haya mawili.

Azma hiyo iliwadia huku Raid Uhuru Kenyatta ambaye yuko nchini  Jamaica kwa ziara ya kihistoria kufanya mashauri na mwenyeji wake Waziri Mkuu Andrew Holness mnao siku ya Jumatatu mchana.

Viongizi hao wawili ambao walikutana katika ofisi za Waziri Mkuu huko Kingston, walishuhudia kutiwa saini kwa mikataba minne ikiwemo  makubaliano kuhusu ushirikiano wa kiufundi katika maswala  ya utalii na nyanja ya michezo, utamaduni na turathi pamoja na mfumo wa ushirikiano kati ya serikali hizi mbili pamoja na mkataba mashauriano ya kisiasa.

Mbali na kusainiwa kwa mikataba hiyo, viongozi hao wawili na jumbe zao walifanya mashauri kati yao ambapo mipango ya suala la kuazisha uunganishwaji wa uchukuzi wa  ndege kati ya Kenya na Jamaica lilijadiliwa.

Viongozi hao wawili walisema usafiri wa ndege kati ya Kenya na eneo la kisiwa hicho cha Carribean utafanikisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi ambao baadaye utasaidia kuboresha ushirikishi wa kiuchumi kwa manufaa ya raia wa mataifa haya mawili.

Kwenye mashauri kati yao, Rais Kenyatta na Waziri Mkuu waliangazia nafasi zilizopo kwa ushirikiano katika usafiri wa anga huku Kiongozi wa Kenya akisema ndege kutoka pwani ya Afrika Mashariki hadi Jamaica utasaidia kuboresha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Carribean na bara la Afrika.

“Shirika letu la kitaifa la ndege limepanga safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi  New York lakini tungependa kuona usafiri wa ndege kutoka pwani ya Afrika Mashariki hadi pwani  ya ya Afrika Magharibi na moja kwa moja hadi Jamaica na baadaye eneo lo la Carribean kupitia Jamaica kama njia ya ukweli ya kuimarisha zaidi ushirikiano wetu,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema njia moja ya hakika ya kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Jamaica ni kuchochea biashara zaidi kati ya mataifa haya mawili.

“Tunastahili kuimarisha biashara zetu  zaidi na kufanya hivyo tutainua uhusiano kati ya raia hadi kiwango kingine. Kenya kwa sasa ni kati ya chumi kubwa zenye nafasi nyingi barani Afrika,” kasema Rais.

Alisema Kenya inahudumu kama kitovu cha  mipango ya  huduma za ugavi na uchukuzi, huduma za  kifedha, ubunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano alipowarai  wawekezji wa Jamaica kuleta rasilimali zao humu nchini.

Viongozi hao wawili  pia walijadili ushirikiano kati ya Kenya na Jamaica kuhusiana na uchumi wa rasilimali za baharini ambao walisema una uwezo mkubwa wa kuzalisha mali na kutoa nafasi za kazi.

Kuhusu masuala ya kimataifa, Rais Kenyatta alisema Kenya inaunga mkono kwa dhati mpangilio wa ushirikiano wa mataifa yanayostawi kwenye mfumo kati ya Afrika na mataifa ya visiwa vya Carribean na akatoa hakikisjo kwa mwenyeji wake kwamba Serikali yake itaendelea kupigia debe kukamilishwa kwa mkataba utakaochukuwa nafasi ya mkataba wa Cotonou utakaokamilika Mwezi Februari mwaka ujao.

Kenya itaandaa Kongamano lijalo la mkataba wa mataifa ya Afrika na visiwa vya Carribean baadaye mwaka huu ambapo Waziri Mkuu Holness anatarajiwa kuzuru Kenya.

Kama mojawapo wa sehemu ya mikataba iliyotiwa saini kati ya Kenya na Jamaica kituo cha Global Tourism Resilience and Crisis Management ambacho kina makao yake katika Chuo Kikuu cha West Indies kitafungua kituo chake cha kwanza karika CHuo Kikuu cha Nairobi.

Kuhusu nyanja ya michezo, viongozi hao wawili walisema Kenya na Jamaica zitashirikiana kuimarisha nyanja hiyo hasa riadha ambapo mataifa haya mawili yanatambuliwa kimataifa huku Kenya ikiongoza katika mbio za masafa ya  kadri na masafa marefu nayo Jamaica ikiweka rekodi ya kila mara kwenye mbio za masafa mafupi.

Waziri Mkuu Holness alisema Kenya na Jamaica zimekuwa na ushirikiano thabiti kuanzia enzi ya Marcus Garvey ambaye mafunzo yake ya umoja wa Afrika yalikuwa na ushawishi mkubwa kwenye juhudi za Kenya za kujikomboa kutoka utawala wa Uingereza miaka ya 1960.

“Uhusiano kati ya Jamaica na Kenya ni thabiti. Imenakiliwa kwamba shujaa wetu wa kwanza wa kitaifa Marcus Mosiah Garvey alikuwa na  ushawishi mkubwa kwa hayati  Mzee Jomo Kenyatta, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa  Kenya ma baadaye Rais wa kwanza,” kasema Waziri Muu Holness.

“Kwa misingi hiyo, pia tunakumbuka hayati  Dudley Thompson kama Wakili wa kwanza wa Jamaica na mtetezi wa Muungano wa  Afrika katika  eneo la Afrika Mashariki. Alijizatiti kumtetea vikali hayati Jomo Kenyatta alipokabiliwa na mashtaka ya uhaini yaliyowasilishwa na Serikali ya kikoloni ya Muingereza,” kasema Waziri mkuu.

Alisema uhusiano thabiti wa kihistoria umetekeleza wajibu mkubwa kwa  ushirikiano kati ya Kenya na Jamaica, akiongeza kwamba mataifa haya mawili sharti yatumie msingi huo bora kubuni ushirikiano thabiti wa kiuchumi kwa manufaa ya raia wao.

Mapema, Rais Kenyatta ambaye ameandamana na Mama wa Taifa  Margaret Kenyatta, alikaribishwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu Holness na Gavana Mkuu Patrick Allen katika sherehe iliyofana ya Kiserikali ikiwemo gwaride kamili iliyoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Jamaica pamoja na kufyatuliwa kwa mizinga 21 baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Manley huko Kingston.

Kesho, Rais lKenyatta atakuwa mgeni wa heshima katika sherehe  za 57 za uhuru wa Jamaica.

Kabla ya maadhimisho ya sherehe za uhuru, Rais Kenyatta atakuwa mgeni wa heshima katika maonyesho ya 67 ya Kibiashara, Kiviwanda na Vyakula mjini Clarendon.

Ziara ya Rais Kenyatta inawadia wakati ambapo kisiwa cha Carribean kinaadhimisha mwaka wa 400 tangu kuwasili kwa watumwa wa kwanza wa Afrika katika eneo la Marekani.

Watetezi wa kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Wafrika wanaoishi ugaibuni na raia wa bara hili wanapigia debe maadhimisho hayo kama mwaka wa kurejea nyumbani.

Rais Kenyatta ambaye ameandamaan na Mawaziri Monica Juma (Mashauri ya kigeni), Amina Mohamed (Michezo) na Najib Balala (Utalii) ni miongoni mwa viongozi  wa kizazi kipya ambao wanaendeleza azma ya Muungano wa Waafrika mbali na kushinikiza  ushirikishi  ili kuboresha ufanisi wa Wafrika wote.

-PSCU