barbados

Kenya kujifunza na Mfumo wa Utoaji Huduma za Afya wa Barbados – Margaret Kenyatta

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta amesema kwamba Kenya iko makini kujifunza kutokana na mfumo wa nchi ya Barbados wa utoaji huduma ya afya kwa wote.

Mama wa Taifa alisema haya alipozuru Hospitali maalumu ya kuwahudumia akina mama na watoto ya Edgar Cochrane Polyclinic, iliyoko Bridgetown, Barbados.

Wakati wa ziara hiyo, Mama wa Taifa alikutana na kutangamana na akina mama waliojifungua karibuni wengi wao wakiwa wametembelea hospitali hiyo ili kupewa huduma za matibabu baada ya kujifungua huku wakiwa na watoto wao wachanga.

Mama wa Taifa ambaye alilakiwa katika hospitali hiyo na  Waziri wa Afya wa Barbados Lucille Moe pamoja na mwenzake wa Habari Dkt. Bany Wand, aliongozwa katika ziara ya hospitali hiyo inayotumika kama mfano wa vituo vya afya bora ya umma huku ikitoa huduma bila malipo kwa akina mama wajawazito na watoto ikiwemo huduma za tiba za meno, lishe bora na huduma za ushauri kwa zaidi ya watu alfu 30 kila mwaka.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mama wa Taifa alisema hospitali hiyo ni mfano bora wa jinsi utaratibu wa huduma ya afya kwa wote unavyoweza kubuniwa.

“Nimeridhishwa na kile nilichoona katika hospitali hii. Huduma za hali ya juu zinazopewa akina mama na watoto wao zapaswa kujumuishwa katika mfumo wa kutoa huduma za afya ya umma kwa wote,” kasema Mama wa Taifa.

Alisema huku Kenya ikianza kutekeleza mfumo wa utoaji huduma za afya kwa wote, nchi hii itajifunza mengi kutoka Barbados hasa katika nyanja za afya ya akina mama na watoto wachanga.

Hospitali hiyo ya Edgar Cochrane Polyclinic ambayo ilianzishwa kama chuo cha kutoa mafunzo ya matibabu mwaka wa 1981, imeimarika zaidi na kuwa mojawapo wa hospitali bora zaidi  ya afya ya umma  katika eneo hilo huku ikiwa na  vituo vingine vinane kote nchini humo vinavyohudumia zaidi ya watu 280,000.

Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa kutoka mataifa 15 wanachama wa Jumuiya na soko huru la Kisiwa cha Caribbean ikiwemo mataifa ya Antigua na Barbuda, Bahamas, Barbados, Belize, Dominica, Grenada, Guyana, Haiti na Jamaica.

-PSCU

Photo Credits: courtesy

Read More:

Comments

comments