Mkenya ahukumiwa maisha eneo la Texas kwa kosa la kunajisi ajuza wa miaka 74

Anthony Mamboleo Nyakeo. PHOTO | Tarrant County, Texas, Sheriff's Office
Anthony Mamboleo Nyakeo. PHOTO | Tarrant County, Texas, Sheriff's Office
Raia mmoja wa Kenya amehukumiwa maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumdhulumu kimapenzi ajuza mmoja mgonjwa, katika eneo la Dallas nchini Amerika.

Tukio hili linajiri miezi michache baada mkenya mwingine kushtakiwa kwa kosa la kumuua mama mzee katika eneo la Texas. Siku ya Alhamisi, Anthony Mamboleo Nyakeo alipatikana na hatia ya kumdhulumu mama mwenye umri wa miaka 74.

“Baada ya tukio hilo wauguzi waliokuwa wakimshughulikia ajuza huyo walipata damu katika chupi yake. Uchunguzi wa matibabu ulionyesha majeraha katika sehemu yake ya siri kuashiria kudhulumiwa kimapenzi. Chembe chembe za DNA zilichukuliwa na uchunguzi ukafanywa uliopelekea kukamatwa kwa Nyakeo," Ofisi ya kisheria ya Dallas aliambia Dallas News.

Nyakeo ambaye alikuwa akihudumu kama muuguzi katika kituo cha afya cha Woodridge Health and Rehabilitation Center eneo la Grapevine, anasemekana kutenda kosa hilo Januari mwaka 2018.

Ajuza huyo ambaye alikuwa mgonjwa alifariki baadaye mwaka huo. Wakati wa kesi hiyo mahakama iliambiwa kwamba Nyakeo alishiriki ngono na mama huyo akifahamu fika kwamba hali yake ya afya haingemruhusu kufanya tendo hilo naye kwa hiari.

“Alikuwa hawezi kuongea, kujilisha au hata kwenda haja pekee yake na alitegemea usaidizi wa wahudumu wa kituo hicho kufanya hivyo," Jordan Rolfe, kiongozi wa mashtaka alisema.

Akijitetea, Nyakeo alikana madai ya kumdhulumu mama huyo, akisema kwamba huenda walichukuwa DNA yake kutoka kwa kondomu aliokuwa ametumia na kumwekea mama huyo.

“Nilimuosha tu na kumpeleka katika eneo la kupata chakula, ” alisema.