Kifo cha rais Nkurunziza, Uhuru atuma risala za rambirambi

Marehemu rais Pierre Nkurunziza
Marehemu rais Pierre Nkurunziza

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia, Jamaa, marafiki na wananchi wa jamhuru ya Burundi kufuatia kifo cha rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Uhuru katika ujumbe wake wa rambirambi siku ya Jumanne, alisema kwamba Nkurunziza alikuwa kiongozi thabiti katika kanda hii aliyehudumia vyema nchi yake na kufanya bidii kuleta amani na ustawi nchini mwake na katika kanda ya maziwa makuu.

Soma pia;

Rais alisema, "Kifo kimeipokonya Afrika Mashariki kiongozi shupavu ambaye mchango wake kuleta utangamano na amani katika kanda hii utakoswa."

Aliomba Mungu kuliwaza familia yake, wananchi wa Burundi na Afrika Mashariki wakati huu mgumu wanapoomboleza kiongozi wao.

Serikali ya Burundi siku ya Jumanne ilitangaza kifo cha rais Nkurunziza kwa kile msemaji wa serikali Willy Nyamitwe alisema ni mshtuko wa moyo.

Soma pia;

Kulingana na msemaji huyo wa serikali Rais Nkurunziza alifariki kutokana na mshtuko wa moyo kinyume na uvumi uliokuwa unaenezwa kuwa huenda alifariki kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Majuma machache yaliopita mkewe rais huyo, Denise Nkurunziza alisafirishwa Nairobi kwa ndege ya shirika la Amref kutoka mji mkuu wa Burundi Bujumbura na kulazwa katika hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi baada ya kuripotiwa kuambukiza virusi vya corona.

Serikali ya Burundi imetangaza siku saba za maombolezi. Rais Pierre Nkurunziza alizaliwa Desemba 18, 1963 na amekuwa madarakani tangu mwaka 2005.