Kimya kimya: Raila arejea nchini kutoka Dubai baada ya matibabu

Raila
Raila
Mwakilishi maalum wa AU Kuhusu miundo msingi Raila Odinga alirejea nchini siku ya Jumapili usiku baada ya kufanyia upasuaji mdogo Dubai.

Raila  aliwasili nchini mwendo wa saa nne usiku Jumapili. Ndege yake  ilitua katika uwanja wa JKIA   usiku, afisa mmoja wa usalama ameliambia gazeti la The Star.

Afisa huyo hata hivyo hakuweza kutoa maelezo zaidi kwa sababu ya utaratibu na itifaki. Star imethibitisha kwamba  ndege hiyo mwanzo iliratibiwa kwenda Lusaka lakini ikaelekezwa kutua Nairobi.

Kiongozi huyo wa ODM Julai Mosi  aliwashukuru wakenya kwa kumuombea apate afueni ya haraka baada ya kupokea matibabu  katika Miliki za kiarabu, UAE.